
GAVANA wa zamani wa Meru, Kawira Mwangaza na mumewe Murega Baichu wamejirudi katika ufugaji wa nyuki na uvunaji wa asali, siku mbili tu baada ya ugavana kumtoka Mwangaza rasmi.
Wawili hao walionekana kwenye shamba lao la nyuki wakitalii mizinga na Mwangaza kuthibitisha kwa Maelezo ya picha kwamba walikuwa katika harakati ya kuvuna asali.
“Jumatano ya kuvuna asali,” Mwangaza alisema.
Gavana huyo wa zamani alifuatisha maandishi hayo na kifungu cha Biblia akionekana kujitoa Imani kwamba licha ya masaibu mengi ambayo yamesababisha kubanduliwa kwake kama gavana, bado ana Imani ya kuiona kesho njema.
“Wafilipi 4:7, “Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Askofu Mwangaza aliongeza.
Kuonekana kwake shambani na mumewe kunajiri chini ya saa 24 baada ya kutoa taarifa kuzungumzia anachokihisi kilichangia kubanduliwa kwake ofisini kama bosi wa kaunti.
Kwa mujibu wake, anahisi kabisa jamii ya Meru imetawalwa na taasubi ya kiume akidai kwamba wanaume wengi vigogo wa kisiasa katika kaunti hiyo walipatwa na mchecheto kuona mama akiwa gavana.
“Ajenda kuu haikuwa kuhusu maendeleo na miradi ya Meru bali ilikuwa ni kuniondoa afisini kwa sababu wapinzani wangu walihisi nitawabwaga katika uchaguzi ujao wa 2027 kutokana na historia yangu ya maendeleo katika Kaunti hii ya Meru nimechapa kazi bila uwoga’’ Mwangaza alisema.
Mwangaza kabla awe Gavana alikuwa mwakilishi wa kike wa Meru ambapo alianza kupalilia uongozi wake ifaavyo na akauchukua Ugavana wa Meru kama muaniaji Huru akiwabwaga washindani wake wa karibu Kama Kiraitu Murungi na Mithiika Linturi.
Hata hivyo, nyota yake ya kisiasa imo katika hatari ya kufifishwa kabisa baada ya mahakama ya juu kuidhimisha uamuzi wa seneti kumbandua ofisini, tumaini pekee likisalia kuwa rufaa yake mahakamani dhidi ya uamuzi huo.
Tayari, Meru imepata gavana mpya – Isaac Mutuma ambaye aliwania na Mwangaza kama naibu wake katika uchaguzi wa 2022 waliposimama kwa tikiti ya chama huru.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!