Peter Salasya, mbunge wa Mumias Mashariki

MBUNGE wa Mumias Mashariki. Peter Salasya ameweka wazi kwamba mazingira ya nyumbani kwake katika kaunti ya Kakamega ni safi licha ya kutokuwa na mke.

Mbunge huyo mcheshi ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa mwiba mchungu kwa kinara wa ODM Raila Odinga alisema haya wakati alikuwa akimkaribisha nyumbani kwake kijana ambaye alichangia pakubwa kampeni zake kwa kutunga wimbo ambao anahisi ndio uliwachochea wapiga kura kukubali sera zake.

Alisema kwamba kijana huyo alipata changamoto kuona nyumbani kwake ni safi na nadhifu licha ya mbunge huyo kutokuwa na mke.

Hata hivyo, Salasya alifichua kwamba ako na kijana wa kiume ambaye anamsaidia katika usafi wa nyumba yake.

“Mwanamuziki alishangaa kupata nyumba iliyopangwa vizuri isiyo na mke hehe ingawa nilimpa changamoto niko na house boy anafanya kazi ya ajabu,” Salasya alieleza.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Katika kipindi cha siku za hivi majuzi, Mbunge huyo amekuwa akikashifu ubia mpya baina ya rais William Ruto na kinara wa Azimio Raila Odinga.

Salasya hata hivyo amejipata akiburuzana mabega na baadhi ya wafuasi wa viongozi hao wawili, jambo ambalo hajalikalia kizembe.

Katika chapisho kwa njia ya video, Salasya aliwataka watu ambao bado wanaunga mkongo Raila Odinga kusitisha ufuasi katika kurasa zake za mitandao, akisisitiza haja ya kuwa na wafuasi wachache ambao wanafuata miongozo yake.

“Kama wewe ni mtu wa nyanza ama mufuasi wake na unaona sikubambi ebu unfollow me right now because you won’t have peace nitakupa depression. Nataka kubaki na wafuasi wachache ambao tunashiriki ideology ya kawaida ...lazima niwatoe ujinga wa huyu baba yenu ambaye amebadili akili zenu. Ametuchezea muda mrefu na lazima tumchezee sasa hivi,” Salasya alifoka.

Mbunge huyo hata alisema kwamba yuko tayari kupokea madhara yoyote yatakayotokana na msimamo wake wa kupinga ubia wa UDA na ODM.

Alisema kuwa haogopi kutolewa katika serikali hiyo jumuishi, akisema lengo ni kuhakikisha wananchi wanafahamu kile alichokitaja kama ukweli.