Geoffrey Mosiria

WAZIRI wa mazingira katika kaunti ya Nairobi Geoffrey Mosiria kwa mara ya kwanza amezungumzia kiini cha ugomvi wake na mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino.

Akizungumza kwenye runinga ya NTV, Mosiria alifichua kwamba bifu kati yake na Owino haijaanza wakiwa viongozi katika nyadhifa tofauti kwenye kaunti ya Nairobi bali ni ugomvi ambao una mizizi yake tangu wakiwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Nairobi.

Kulingana na Waziri huyo wa kaunti, walianza kugombana na Babu Owino wakati wote walijikuta wakiwa washindani wa wadhifa wa rais wa wanafunzi katika chuo cha Nairobi.

Hata hivyo, Babu Owino ambaye anajulikana kuwa kiongozi wa wanafunzi chuoni Nairobi kwa muda mrefu alimshinda Mosiria, uchaguzi ambao Waziri huyo wa kaunti anadai kwamba ulihitilafiwa kwa faida ya Owino.

“Bifu yangu na Babu inarudi nyuma hadi tukiwa chuoni, Babu anaamini kwamba Mosiria hawezi kumshinda. Niliwania dhidi ya Babu Owino katika uchaguzi wa SONU (chuoni Nairobi) na kura ziliibwa kwa faida ya Babu kwa sababu yeye alikuwa ni kibaraka wa uongozi wa chuo. Na bifu hiyo bado ingalipo,” Mosiria alisema.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Mosiria alisema kwamba licha ya wote kuondoka katika siasa za chuoni na kujipata katika njia tofauti katika uongozi wa kaunti ya Nairobi, bado anahisi Owino anahisi kuwa yeye ni tishio kwake.

“Hapa sasa mimi ni afisa mkuu wa mazingira ya kaunti chini ya gavana Sakaja na Babu ni mbunge Embakasi Mashariki. Lakini bado anahisi kwamba mimi ni tishio kwake na pengine anahisi kwamba huenda nitakata kuwania ubunge katika eneobunge lake.”

Afisa huyo wa mazingira hata hivyo alimshauri Owino kutokuwa na wasiwasi anapomuona akifanya mashauriano na vijana katika eneobunge lake wakati amezuru kufanya angalizo kuhusu uchafuzi wa mazingira na kumtaka kuacha kuingilia utendakazi wa kaunti.

“Lakini ningependa kumwambia ndugu yangu, hudumia watu wako kwa heshima na taathima, fany kazi ambapo Mungu amekupa na achene kuingilia utendakazi wetu kama maafisa wa mazingira kwa kuchapisha picha ambapo kuna takataka. Badala yake wewe kama kiongozi toa suluhisho,” Mosiria alimaliza kwa kumshauri Owino.