
MMILIKI wa hisa chache katika klabu cha Manchester United, bilionea Jim Ratcliffe amekiri kwamba anahisi anguko kuu la klabu hiyo lilijiri wakati wa uamuzi wa kumtafuta mrithi wa meneja wa muda mrefu, Sir Alex Ferguson.
Akizungumza na jarida la The Times, Ratcliffe alisema kwamba Manchester United ilipoteza dira ilipoamua kumleta David Moyes – kutoka Everton kipindi hicho – kuja kuvaa viatu vya Alex Ferguson aliyekuwa anastaafu.
Hata hivyo, aliweka wazi kwamba kauli yake haikulenga kumdhalilisha kwa njia yoyote Moyes, akimsifia kama kocha mahiri lakini akasema anahisi hakustahili kuvivaa viatu ‘vikubwa’ vya Ferguson.
"Angalia, nampenda David Moyes, na nadhani ni meneja mzuri sana, lakini kutoka kwa Sir Alex Ferguson hadi Moyes si mahali ambapo ningeenda," Ratcliffe aliambia The Times.
"Moyes aliingia kwenye viatu vya Ferguson, ambaye ameshinda Ligi Kuu mara 13, ambaye alishinda Ligi ya Mabingwa mara mbili na kisha unamkabidhi kocha ambaye hajawahi kuwasimamia wachezaji wakubwa na hajawahi kushinda chochote.”
"Si lazima awe na utu wa kusimama mbele yao wote. Na sidhani kama Real Madrid wangefanya chaguo hilo kama kocha."
"Ukiangalia makocha, klabu haiwezi kuwa sawa kila wakati, lakini walipaswa kupata mtendaji mkuu bora duniani, na kocha bora zaidi duniani, kwa sababu Manchester United ni klabu bora zaidi duniani. Badala yake walikosa maamuzi yote mawili.”
Moyes alikaa chini ya mwaka mmoja dimbani, na kuiongoza United kufikia kile ambacho wakati huo kilikuwa kilele cha pointi chache zaidi kuwahi kutokea kwenye Premier League.
Tangu Moyes, kumekuwa na mameneja tisa zaidi wa United - wawe wa kudumu au washikilizi wa muda.
Bado, hakuna aliyeweza kuiongoza klabu hiyo hadi pale Fergie alipoiacha: Ubingwa wa Ligi Kuu.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!