
BINTI mwenye umri wa miaka 13 kutoka mtaa wa Umoja jijini Nairobi ambaye amekuwa aki’trend kutokana na sauti yake ya kufana katika tungo zake za muziki amefunguka kwamba ana azma ya kusomea uimbaji wa muziki wa injili.
Ellyne Miracle, msichana anayesoma katika Gredi la 8 aliweka wazi kwamba kando na kujikita kwa bidii masomoni, lakini bado analenga kuwa miongoni mwa wanamuziki shupafu wanaoeneza injili kupitia nyimbo.
Binti huyo aliweka bayana kwamba amekuwa mfuasi mkubwa wa nyimbo za injili kwa muda mrefu, huku akiwataja wasanii kama vile Mercy Masika kutoka Kenya na Israel Mbonyi kutoka Rwanda kuwa vichocheo vikuu vya talanta yake.
“Naitwa Ellyne Miracle, mwanafunzi wa Gredi la 8 mwenye umri wa miaka 13. Nina msukumo katika uimbaji na msukumo huu nimekuwa nao tangu nikiwa mdogo.”
“Kilichonichochea kupenda uimbaji wa miziki ya injili ni baadhi ya wasanii wa injili tulio nao hapa nchini Kenya kama vile Mercy Masika, Size 8 na wengine kama Israel Mbonyi kutoka Rwanda,” alisema.
Licha ya udogo wake kiumri, binti huyo wa ajabu alifichua kwamba mapenzi yake kwa muziki wa injili yamemfanya kutanua wigo hadi katika wanamuziki wa kimataifa kama vile Cece Winans na Kathy Franklin – wote kutoka Marekani.
Binti huyo ambaye amekuwa akijireko nyumbani akiimba sasa anaomba msaada wa kupata ufadhili katika shule ya muziki ili kupata kufunzwa jinsi ya kunyoosha sauti yake lakini pia jinsi ya kutumia ala mbalimbali kucheza muziki.
“Ninachoomba ni kufadhiliwa katika shule ya muziki ambapo nina uhakika nitaboresha sauti yangu ya uimbaji kwa sababu ninataka kuimba kwa sauti nzuri na kuwamotisha wengi jinsi ambavyo hawa wasanii wangu pendwa niliowataja wamenichochea kimuziki,”Ellyne alisema.
“Na pia katika hiyo shule nitakuwa na uwezo wa kukuza talanta yangu lakini pia nitaweza kuimarika katika kutumia ala zote za kucheza muziki,” aliongeza.
Ellyne Miracle pia hakufutili mbali uwezekano wa kuwa mkuza maudhui ya kuwasongeza watu karibu ya Uungu.
Haya hapa mazungumzo yake:
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!