
SENETA wa Kakamega, Boni Khalwale ametoa wito kwa vijana wa marehemu mbunge wa Malava, Moses Malulu Injendi kuhakikisha wamezaa watoto wa kiume na kuwaita jina la baba yao haraka iwezekanavyo.
Akizungumza Jumanne wakati wa halfa ya mazishi ya mbunge huyo, Khalwale alisema kwamba anafahamu fika vijana wa Injendi wamechoka lakini akawapa changamoto ya kutolala kabla ya kuzaa watoto watakaoitwa Malulu Injendi.
“Vijana wa Injendi, najua mmechoka, lakini nawaomba msiende kulala. Nataka kuanzia leo kabla ulale, uhakikishe umezaa Moses Malulu Injendi,” Khalwale aliwarai.
Khalwale anayefahamika kwa kuwa na watoto wengi alisema ikiwa watashindwa kuzaa watoto na kuwaita Injendi basi yeye atarudi kutoka maisha ya ustaafu na kuingia uwanjani kucheza hadi afunge bao la kuzalisha mtoto atakayeitwa Malulu Injendi.
“Malulu alikuwa ni mtu mzuri na nataka watoto wake waonyeshe hiyo heshima ili nikija hapa kama ambavyo nimekuwa nikija nitakuwa ninahesabu Malulu wengine wengi.”
“Msipofanya hivyo hata mimi naweza kasirika niende nichukue viatu kutoka kwa stoo nianze kucheza mpira mpaka nipate mtoto nitakayemuita Malulu Injendi,” Khalwale alisema.
Khalwale alifichua kwamba Injendi si tu alikuwa kama rafiki yake lakini pia alikuwa ni mtoto wake kisiasa, akieleza jinsi alimshawishi kuingia katika siasa mwaka wa 2011.
Kando na kumuomboleza Injendi, Khalwale alimpa matumaini rais William Ruto akimhakikishia kwamba atamaliza hatamu yake ya mihula miwili ofisini bila wasiwasi.
“Ninajua desturi ya siasa za Kenya chini ya katiba mpya, na ningependa nikutulize nisaidie hiyo desturi marafiki zako na wapinzani wako. Desturi ya Kenya since 1992 ni kwamba rais sharti amalize mihula miwili. Na mimi siamini kwamba itakuwa tofauti ifikapo 2027. Wewe utachaguliwa tena,” Khalwale alimuasa Ruto.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!