
MWANZILISHI wa chama cha INJECT, Morara Kebaso ametangaza kwamba chama hicho rasmi kimejiunga na muungano wa upinzani unaoandaliwa.
Kupitia ukurasa wake wa X, Kebaso alieleza kwamba INJECT sasa ni moja kati ya Vyama tanzu vitakavyoendelea kuikosoa serikali, lengo likiwa si kutupiana lawama bali kutafuta suluhisho.
“Chama cha INJECT kimejiunga na muungano wa upinzani. Kazi yetu sio kulalamika juu ya hili au lile na yeye. Dhamira yetu ni kutoa suluhisho,” Kebaso alisema.
Aidha. Mwanaharakati huyo alisema kwamba wataendelea kutetea haki za wananchi haswa vijana wa Gen Z ili kupata fursa za ajira nchini.
Alihakikishia wafuasi wake kwamba wakiendelea na harakati za kuikosoa serikali kwa njia ifaayo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, mrengo wao utaibuka na ushindi na kutengeneza serikali mpya ambayo kulingana na yeye itawapa vipaumbele vijana wa Gen Z.
“Kuhakikisha kwamba maadili na misingi ya utawala bora inaheshimiwa. Tunataka haki na fursa kwa vijana kuishi, kufanya kazi na kukua. GenZs, sisi ni wapinzani sasa; baada ya muda mfupi tutakuwa serikali. Wacha tuingie chumbani kwa ujasiri na tubadilishe jinsi mambo yanafanywa kutoka ndani. Kama kiongozi wako, ninajitolea kuwa icon bora ya uadilifu,” Kebaso alisema.
Tangazo lake linajiri wiki moja baada ya kuhudhuria hafla ya kuzindua upya kilichokuwa chama cha NARC-K kilichozaliwa upya kuwa PLP.
Kebaso pia alionekana katika hafla nyingine ambayo ilihudhuriwa na viongozi wanaoipinga serikali akiwemo Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka, Eugene Wamalwa, Martha Karua miongoni mwa wengine.
Hata hivyo, baada ya kutangaza kujiunga na vigogo hao wa kisiasa, sasa inasubiriwa kuonekana ikiwa Kebaso ataendelea na azma yake ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!