
SHIRIKISHO wa mawakili wa kike nchini Kenya, FIDA imetoa tamko la kulaani vikali video ambayo ilizua minong’ono mitandaoni wiki jana ikionyesha ajuza mmoja akichomwa moto kanisani kama njia ya kufukuzwa mapepo katika maisha yake.
Video hiyo ilirekodiwa katika kanisa moja kaunti ya Bomet ambapo makumi ya waumini walionekana kumzunguka ajuza huyo nje ya jengo la kanisa huku wakimketisha kwenye moto.
Katika taarifa yao, FIDA imelaani kitendo hicho ikisema kuwa wana ripoti kutoka kwa polisi kwamba kanisa hilo ndilo pia limesemekana kuwachapa wanawake waumini.
“FIDA Kenya imechukizwa na video inayosambaa ya mwanamke mzee akiteketezwa motoni na washirika wa kanisa la Bethel for Jesus Ministry International huko Kapkwen kaunti ya Bomet kama njia ya kufukuza mapepo mabaya kwake.”
“Cha kushangaza ni ujasiri ambao baadhi ya waumini walikuwa nao kusimama mbele ya kamera kujipiga kifua kuhusu tukio hili,” FIDA walisema katika barua yao.
Shirikisho hilo lilitoa wito kwa vyomvo vya usalama kukomesha vitendo kama hivyo, wakisikitika kwamba wanawake bado wanaendelea kudhulumiwa hadi katika Maeneo ya ibada ambapo wanastahili kupata msaada.
“Jambo la kujutia sana kwamba wanawake bado wanaendelea kupokea manyanyaso ya kijinsia hata katika Maeneo ambayo ni ya kuabudu. Tunatoa wito kwa kamishna wa kaunti ya Bomet kuweka mikakati ya kuwalinda wanawake dhidi ya aina zote za dhuluma,” waliongeza.
Pia walitoa wito kwa ODPP kuharakisha katika kuandaa mashtaka dhidi ya wahusika kama njia moja ya kupunguza visa vya aina hiyo dhidi ya wanawake.
FIDA ilisema kwamba visa vya dhuluma za kijinsia haswa dhidi ya wanawake vimekuwa katika hali ya ongezeko katika miaka ya hivi karibuni, wakitolea mfano tukio la miaka miwili iliyopita la huko Shakahola ambapo idadi ya watu wengi waliofukuliwa baada ya kujitesa njaa hadi kufa ilikuwa ya wanawake na watoto.
“FIDA Kenya tunasisitiza haja ya kuwalipa watu mazingira magumu haswa wanawake na watoto dhidi ya kutumiwa vibaya na dini,” walisema.
Shirika hilo pia lilimaliza kwa kutoa himizo kwa bunge la kitaifa kupitisha sheria ya kudhibiti shughuli za dini humu nchini.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!