Facebook

KAMPUNI mama ya Facebook, Meta imetangaza kuanza kutekeleza kanuni ya kufuta kabisa video za moja kwa moja kwenye jukwaa hilo kila baada ya siku 30.

Katika chapisho kwenye tovuti rasmi ya Meta, kampuni hiyo ilisema kwamba sasa watumizi wa Facebook wanaofanya video za moja kwa moja watakuwa wanazipoteza kabisa pindi zinapomaliza siku 30.

Kanuni hiyo ilianza kutekelezwa Februari 19, ambapo Facebook ilisema itakuwa inawatumia wamiliki wa video barua pepe kuwajulisha kuwa video zao zinakaribia kumaliza siku 30, hivyo kufgutwa kabisa.

“Kuanzia tarehe 19 Februari, video za moja kwa moja zinaweza kuchezwa tena, kupakuliwa au kushirikiwa kutoka kwa Kurasa za Facebook au wasifu kwa siku 30, na baada ya hapo zitaondolewa kiotomatiki kwenye Facebook,” walitoa sasisho.

Hata hivyo, walisema kuwa barua pepe itampa mmiliki wa video nafasi ya kukata rufaa ya kuongezewa siku zaidi kabla ya video zake kufutwa.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

 “Video za moja kwa moja ambazo zimehifadhiwa zaidi ya siku 30 kwa sasa zitaondolewa kwenye Facebook. Kabla ya kumbukumbu zako za moja kwa moja za video kufutwa, utaarifiwa kwa barua pepe na katika programu, na kuanzia hapo utakuwa na siku 90 za kupakua au kuhamisha maudhui yako.”

Meta ilisema kwamba itakuwa inakubalia rufaa ya hadi miezi 6 na baada ya hapo utazipoteza video zako zote za moja kwa moja kama hutakuwa umezihifadhi kwa kuzipakua.

“Iwapo unahitaji muda wa ziada ili kupakua video zako za awali za moja kwa moja, tunatoa chaguo la kuahirisha ufutaji kwa miezi sita ya ziada. Baada ya kipindi hicho, ikiwa hutafanya chaguo, video zako za awali za moja kwa moja zitaondolewa na hazitapatikana tena.”

Facebook walitetea hatua hiyo wakisema kwamba ni njia moja ya kuboresha jinsi watumizi wanaburudika na mitandao huo kuambatana na video za usasa zaidi.

“Mabadiliko haya yataoanisha sera zetu za uhifadhi na viwango vya sekta na kusaidia kuhakikisha kuwa tunatoa hali ya utumiaji iliyosasishwa ya video za moja kwa moja kwa kila mtu kwenye Facebook.”

Facebook walitangaza kuanzisha njia zingine zitakazowawezesha watu kupakua video zao kwa wepesi zaidi katika siku za hivi karibuni.

“Mchakato wa kufuta utafanyika kwa mawimbi katika miezi ijayo, na tunatoa zana mpya kwa watu kupakua video zao za awali za moja kwa moja kabla hazijafutwa hatua kwa hatua.”