Cosmas Choi

COSMAS Choi, Mkenya anayeishi nchini Marekani na ambaye amekuwa akitoa ukosoaji mkubwa kwa uongozi mbalimbali humu nchini kupitia mitandao ya kijamii ametangaza rasmi nia yake ya kujiunga kwenye siasa za Kenya.

Kupitia kurasa zake kwenye mitandao ya kijamii, Choi alichapisha ujumbe akieleza kwamba ameacha kazi yake ya kuendesha malori nchini Marekani na sasa macho yake yanaelekezwa katika siasa za Kenya.

Cosmo Choi alifichua kuwa kazi hiyo ya kuendesha malori nchini USA ilikuwa inamlipa zaidi ya shilingi milioni 2 kwa mwezi lakini sasa hana budi kwani ameitikia wito wa kuhudumia Wakenya bungeni.

Alifichua kuwa atakuwa debeni katika uchaguzi mkuu wa 2027 akiwania ubunge katika Eneobunge la Embakasi Mashariki, ambapo mbunge wa sasa ni Babu Owino.

“Nimejiondoa hivi punde kutoka kwa kampuni hii ya kimataifa ya Ryder18 wheels, ninagombea ubunge wa Embakasi Mashariki 2027. Ujumbe umeidhinishwa. Kazi hii Inalipa zaidi ya Ksh 2m kwa mwezi,” Cosmas Choi aliandika kwenye Facebook.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kufikia sasa, haijabainika wazi ikiwa mbunge wa sasa wa Embakasi Mashariki, Babu Owino atakuwa analenga kutetea wadhifa wake kwa mara ya tatu mtawalia.

Owino amekuwa mbunge wa Eneobunge hilo tangu mwaka 2017 kwa tikiti ya chama cha ODM lakini katika siku za hivi karibuni, wandani wake wamekuwa wakidokeza kuwa huenda akajitosa katika kinyang’anyiro cha ugavana Nairobi.

Ikiwa Owino atawania ugavana, basi atakuwa na kibarua kigumu kwani gavana wa sasa Johnson Sakaja anatarajiwa kutetea wadhifa huo alioshinda katika uchaguzi wa Agosti 2022 kwa tikiti ya UDA.