
SIKU moja baada ya uvumi wa DJ Mo na mkewe Size 8 kufanya harusi ya kisiri katika Maeneo ya Sigona kaunti ya Kiambu, mchungaji Size 8 amevunja kimya kuhusu tukio hilo.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Size 8 alifichua kwamba tukio hilo lilikuwa kufanya upya viapo vyao vya ndoa mnamo Februari 18.
Mchungaji Size 8 alimshukuru Mungu kwa matukio yote ambayo yametukia katika uhusiano wao wa zaidi ya miaka 10 sasa.
“Siku hii ❤️18:02:25 ❤️Mungu alifanya hivyo na tukafanya upya viapo vyetu vya ndoa ? .....kwa neema na rehema za Mungu tumeona urejesho wa Mungu katika ndoa yetu.....kile ambacho Mungu hawezi kufanya hakipo.....Je, hili ndilo tendo la Bwana, nalo ni la ajabu machoni petu......."
Japo ilikuwa harusi ya kisiri, Size 8 alisema mashabiki wake watapata nafasi ya kipekee kuona matukio hayo kwenye YouTube Alhamisi hii.”
“Kesho kwenye youtube ya murayas tunayofuraha kukushirikisha video ya yale Mungu amefanya...mtu asherehekee jina la Yesu Kristo pamoja nasi.... uuuuuwwiii haleluya...... Yesu Kristo ni Bwana!” Size 8 alichapisha.
Sherehe ya harusi ilipambwa na marafiki zao wa karibu na familia ambao wote walikuwa katika shangwe huku wawili hao wakila kiapo cha harusi.
Miongoni mwa walioonekana kwenye harusi hiyo ni watu mashuhuri kutoka tasnia ya kidunia na ya injili.
Wageni wa harusi walikuwa wamevaa nguo nyeusi. DJ Mo alikuwa amevalia suti nyeupe huku Size 8 akitamba na gauni zuri la Light-pink.
Harusi hiyo imekuja siku chache baada ya DJ Mo na Size 8 kuweka hadharani kuwa wamerudiana baada ya kuachana kwao kulikotangazwa mwaka jana.