
Kwa mara ya kwanza serikali ya Kenya Kwanza imekiri kuwa bima mpya ya Afya ya SHA inakabiliwa na changamoto za kifedha hali ambayo imeathiri pakubwa huduma zake.
Siku ya Jumatano Wizara ya Afya iliwaomba Wakenya kuchangia Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) ili kuhakikisha huduma za matibabu hazikatizwi.
Katika mkutano wa kila wiki waziri wa Afya Deborah Barasa na Mkurugenzi Mkuu wa Afya Dkt Patrick Amoth waliangazia matatizo ya kifedha katika Hazina ya Bima ya Afya ya Jamii (SHIF).
Kulingana na maafisa wa afya, suala kuu ni michango ya Wakenya katika mpango unaonuiwa kutoa huduma za matibabu kwa wote. Kati ya Wakenya milioni 19.4 waliosajiliwa kwenye SHA, ni milioni 3.3 pekee wanaochangia mpango huo.
"Huduma za afya ni ghali na hatuwezi tu kuwa na wale walio katika ajira rasmi kubeba mzigo wa wakazi wengine wa Kenya," alisema Amoth.
Amoth aliongeza kuwa kushindwa kwa wakenya kutoa michango kunasambaratisha utoaji wa huduma na kuwataka wakenya wote kushiriki jukumu hilo.
"Tunatoa wito kwa kaunti kuhakikisha Wakenya wengi wanajiandikisha kwa SHA, huku maeneo kame yakiongoza kwa usajili wa chini," alisema.
Katika kutekeleza azma yake ya kutoa huduma za afya jumuishi kwa Wakenya, kufuatia malalamiko kuhusu hitilafu za mfumo na makato, Wizara ya Afya imeanzisha Jopo la Ushauri ambalo litakuwa na makao yake katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Jopo hilo , miongoni mwa majukumu mengine, litakagua manufaa ya bima hiyo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, zaidi ya Wakenya milioni moja wamepata huduma za afya ya msingi tangu Oktoba 2024. Katika kupunguza muda wa uidhinishaji wa awali, ambao ulikuwa mojawapo ya changamoto kuu, Waziri alisema muda wa kushughulikia maombi ya idhini ya awali umepungua kutoka saa 10 hadi takriban saa 1 dakika 15.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!