Rais William Ruto na Mbunge Eric Wamumbi

Siku ya Jumapili, Februari 9, kulikuwa na matarajio makubwa kwamba Rais William Ruto angehudhuria ibada maalum katika kanisa la Victors Chapel katika mji wa Karatina, eneo bunge la Mathira, kaunti ya Nyeri.

Rais alitarajiwa kupamba hafla ya kusherehekea miaka 25 ya kanisa hilo linaloongozwa na William Githinji lakini akakosa kuonekana huko huku kukiwa na tetesi kwamba angepokea mapokezi mabaya. Hii ni kutokana na eneo la Mathira kuwa uwanja wa nyumbani wa aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua, ambaye kwa sasa amemfanya kuwa adui yake mkubwa.

Mbunge wa Mathira Eric Wamumbi hata hivyo alipokuwa akihutubia wanahabari nje ya kanisa hilo alidai kuwa rais alikuwa ameamua kumtuma yeye na seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga kumwakilisha kwani alikuwa na mkutano mwingine muhimu.

“Siku ya Ijumaa alinipigia simu mimi na seneta Wamatinga na kutuambia kutokana na vita vya Goma, Kongo, ameitisha kikao cha marais wa nchi zote za Afrika Mashariki kwa vile yeye ndiye mwenyekiti, ili wajadiliane namna ya kutatua vita. Kama mwenyekiti, ana wajibu,” Wamumbi alisema.

Mbunge huyo wa muhula wa kwanza alidai kuwa rais alisafiri kwa ndege hadi Tanzania siku ya Ijumaa baada ya kukamilisha safari yake katika eneo la Kaskazini Mashariki.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Wamumbi aliongeza kuwa amiri jeshi mkuu alishindwa kufika kwa Mathira kwa kuwa bado alikuwa amekwama Tanzania ambako alikuwa akishirikisha viongozi wengine wa Afrika.

“Bado yuko Dar es Salam. Angekuja. Mimi niko hapa, tuko hapa na tumeleta zawadi yake kwa kanisa hili. Sababu iliyomfanya asije ni kwa sababu yuko Dar es Salam, Tanzania ambako ana kikao na marais wengine,” alisema.

Rais William Ruto amekaa siku chache zilizopita nchini Tanzania ambako kuna mkutano kati ya viongozi wa Afrika Mashariki na nchi za Afrika Kusini.

Rais huyo wa tano wa Kenya hajaonekana katika mkutano wowote wa hadhara katika eneo la Mlima Kenya katika muda wa miezi kadhaa iliyopita huku hali hiyo ikihusishwa na uhasama dhidi yake katika eneo hilo.