KATIKA kipindi cha Patanisho kwenye Radio Jambo, kijana mwenye umri wa miaka 23 kwa jina Moses Amadi, Mganda anayefanya kazi nchini Kenya alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mpenzi wake Rose Ojema mwenye umri wa miaka 21.


“Nilikosana na Bibi yangu on Julai 2022 kwa sababu ya ulevi. Mke wangu alikuwa Mtu mwenye anaenda kwa baa na kukaa huko sana na Marafiki zake hadi analala huko na saa zingine kurudi nyumbani very late. Kwa hivi sasa niko maeneo ya Kiambu na yeye pia naskia ako Kiambu upande ya Majani,” ujumbe wa Amadi ulisema.


Amadi alisema kwamba ni yeye mwenyewe aliamua kumuacha Ojema kwa sababu alikuwa akitoka na kulala nje huku akiwa ameacha nyuma mtoto wa miezi 6.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Mke wangu alikuwa akienda harudi sasa nikaamua tuachane anakuja usiku nikaamua nimuache na akaenda akaniachia mtoto akiwa na miezi 6… nikachukua mtoto nikapeleka nyumbani saizi nampigia simu ananiambia anataka kurudi namwambia siwezi kubali….”


Baada ya kukatisha mahusiano, Amadi alisema alimrudisha mtoto wake nyumbani kwa wazazi wake lakini sasa anataka kurudiana na Ojema kwa sababu ya mtoto.


Mwanamume huyo alisema kuwa anataka kurudiana na mama mtoto wake kwani sasa mtoto ana miaka 3 na ameanza kuuliza maswali kuhusu aliko mama.


“Nataka kuongea na yeye nione kama tunaweza sameheana… juu mtoto sasa amekuwa mkubwa anataka kuona mamake na mimi namwambia sijui pahali alienda, sasa ana miaka 3…nataka aone mtoto na pia tunaweza rudiana,” Amadi alisema.


Kwa upande wake, Rose Ojema alifichua kwamba sababu ya kutorudiana na Amadi ni kwamba alioa na yeye pia akaamua kuolewa kwingine.


“Yeye alioa na mimi pia nikaamua kuolewa lakini sasa hivi niko nyumbani na ningependa kusikia anasemaje,” Ojema alisema.


Baada ya wawili hao kuzungumza, Amadi aliweka wazi nia yake kwamba angetaka warudiane na Ojema akamtaka kumpigia kwa simu yake ili wayamalize.


Licha ya kuolewa tena, Rose Ojema alisema baada ya ndoa hiyo kuvunjika na kurudi nyumbani, ako tayari kurudiana na mume wa kwanza, ikiwa mume mwenyewe yuko tayari.