MAJIVU ya mwili wa aliyekuwa mwanzilishi wa klabu ya soka ya Mathare United FC, Bob Munro yatanyunyizwa katika makao makuu ya akademia ya MYSA baada mabaki yake kuchomwa Jana Jumanne.


Haya ni kwa mujibu ya taarifa iliyochapishwa na klabu hiyo kwenye mitandao yao ya kijamii.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kunyunyizwa kwa majivu ya mabaki ya Munro kutakuwa njia moja ya kuheshimu matakwa yake aliyoyanakili kabla ya kufa.


“Mwenyekiti wetu mpendwa Bob Munro alizikwa leo katika Ukumbi wa Maiti wa Kariokor kwa ibada ndogo ya kibinafsi kwa familia yake na marafiki wa karibu. Kulingana na matakwa yake, majivu ya Bob yatatawanywa na familia katika makao makuu yetu ya MYSA Kenya,” Mathare United walitaarifu.


Bob Munro alifanyiwa ibada ya maziko katika masihara ya Kariakor jijini Nairobi baada ya msururu wa ibada zingine zilizofanyika tangu Jumamosi alipotolewa katika makafani.


Awali, ibada ya misa ya wafu kwa ajili ya mwenyekiti huyo wa Mathare United ilifanyika katika kanisa la St Andrew mnamo Januari 27.


Mkewe, Ingrid Sofia Munro alitoa risala za kugusa hisia wakati wa ibada ya wafu kwa marehemu mumewe na mwanzilishi wa Chama cha Michezo cha Vijana cha Mathare (MYSA) Bob Munro.


Ingrid aliwaambia mamia ya waombolezaji waliojitokeza kwa ajili ya ibada ya mazishi jinsi marehemu Munro alifariki mikononi mwake walipokuwa wakisubiri gari la wagonjwa kumpeleka hospitalini.


"Alikuwa akiumwa kwa muda na siku hiyo alizidi kuwa mbaya na akapiga simu ambulensi. Wakati tunasubiri, nilikuwa nimemshika mikononi mwangu na akasema 'Oh Ingrid nakufa'. Lakini nilijibu 'Hapana, hauko' kisha akanyamaza.”


“Nilidhani labda alikuwa amepoteza fahamu. Madaktari walipokuja na kumwangalia walithibitisha kuwa alikuwa amefariki,” aliwaambia waombolezaji.


Bob aliaga dunia kwa amani nyumbani kwake Nairobi siku ya Jumapili, 19 Januari. Alikuwa 82.