MFANYIBIASHARA wa magari anayepitia wakati mgumu, Khalif Kairo amewarudia marafiki zake na mashabiki wa mitandaoni kuwaomba msaada wa mchango kuikomboa kampuni yake.


Kairo ambaye alitiwa mbaroni kwa mara nyingine mapema wiki hii aliwataarifu watumizi wa mitandao wa X akiwaomba mchango ili kuinusuru kampuni yake – Kai&Karo ambayo inachungulia kaburi.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Alisema kwamba ni wakati wa watu kujitokeza kimasomaso ili kumsaidia kifedha kupambana na watu wa gizani ambao wanajita juhudi katika kuipoteza kabisa kampuni yake.


“Ninawaomba moja kwa moja wafuasi wangu, marafiki, wateja wa zamani na washirika wangu kutumia kiasi chochote wanachoweza na kutupa nafasi ya kupambana dhidi ya vikosi visivyojulikana vinavyoharibu kampuni yangu,” Kairo aliomba.


Aliweka paybill kwa ajili ya michango akisema kwamba baada ya misukosuko yote kutulia, ataeleza kwa hisabati jinsi michango hiyo ilifanya kazi katika kuipa uhai tena Kai&Kairo.


“Mapato yanaweza kutumwa kwa @kai_and_karo akaunti hapa chini.  Huu sio uwekezaji bali ni mchango. Punde tu vumbi likitimka, tutatoa tamko na ufuatiliaji wa ukaguzi wa jinsi tutakavyotumia pesa zilizopatikana katika kuokoa kampuni yetu,” Kairo aliwasihi mashabiki na marafiki.


Alisema kwamba leo hii Jumatano anatarajiwa kuwasilishwa mahakamani kulishwa kiapo kabla ya kufunguliwa mashtaka anayotuhumiwa kutekeleza kwa kukosa kuwafikishia wateja magari waliyonunua kupitia kwa kampuni yake.


“Kwa sasa niko katika mahakama za Milimani na nitawasilishwa kwa ajili ya kujibu maombi hivi karibuni. Nimekuwa na biashara ya kuvutia kwa miaka kumi bila kesi za uhalifu zinazohusu magari na maelfu ya watu wamefanikiwa kununua magari kutoka kwangu,” alisema kwa kutamba.


Kairo aliarifu wateja wake kwamba ofisi za kampuni yake zote zimesalia kufungwa kwani alikesha usiku kucha katika kituo cha polisi baada ya kukamatwa Jumanne alipokuwa akitoka mahakamani.


“Jana baada ya kuhudhuria shauri katika mahakama za Milimani, nilikamatwa tena na kushikiliwa katika kituo cha polisi cha Parklands usiku kucha kwa suala lingine.  Tumejaribu kila kitu katika uwezo wetu kujaribu kutatua masuala haya kwa amani, kuhakikisha tunatuma bidhaa lakini utangazaji mbaya wa vyombo vya habari na ushiriki wa polisi mara kwa mara unatuweka kwenye kina kirefu na kuathiri sana uwezo wetu wa kufanya kazi. Ofisi zetu zote zimefungwa kwa sasa,” Kairo alieleza.