Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf, ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), amekanusha madai ya kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.

Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, Ali Youssouf aliweka wazi kuwa bado yuko imara kwenye kinyang'anyiro hicho.

Waziri huyo ndiye mpinzani mkuu wa mgombea wa Kenya Raila Amollo Odinga.

"Kuweni na uhakika marafiki wapendwa na wafuasi, bado niko kwenye kinyang'anyiro na ninaendelea vyema hadi sasa," Ali Youssouf alisema kupitia akaunti yake ya Twitter.

Afisa huyo wa serikali ya Djibouti alipuuzilia mbali uvumi wote kuhusu yeye kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho ambao uliibuka mapema wiki hii.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

"Msijisumbue na habari za uwongo, ni jaribio dogo la wapinzani wangu kuwavuruga wafuasi wangu na kuwapotosha," alisema.

Ali Youssouf alitoa maoni hayo baada ya kufanya ziara katika nchi jirani ya Tanzania ili kuelezea msaada wake.

Katika ziara yake siku ya Alhamisi, alikutana na Rais Samia Suluhu Hassan na kuwasilisha kwake ilani yake ya uchaguzi.

"Nilipata heshima na baraka kupokelewa asubuhi ya leo na Mhe Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," alisema baada ya mkutano wake na Samia.

Siku hiyo hiyo, pia alifanya mkutano na waandishi wa habari na vyombo vya habari vya Tanzania ili kuwasilisha maono na matarajio yake kwa bara la Afrika.

Mapema wiki hii, tetesi ziliibuka kuwa raia huyo wa Djibouti alijiondoa katika kinyang'anyiro cha uenyekiti wa AUC na badala yake akajitolea kuunga mkono azimio la Raila Odinga.

Pia kulikuwa na madai ya uwongo ya yeye kuhongwa ili aache kinyang'anyiro.