NA GREGORY MULEMI

Mwanzilishi wa Mathare Youth Sports Association (MYSA) Robert Munro anayejulikana sana kama Bob Munro aliaga dunia Jumapili nyumbani kwake Westlands, Nairobi.

Bob Munro alikuwa na roho ya utu na alikuwa kama mzazi na kinara wa matumaini kwa wale ambao aliwasaidia kutimiza ndoto yao ya kimaisha hasa kwa vijana katika vitongoji duni vya Mathare na kwingineko jijini Nairobi.

Mchango wa Bob katika soka ya Kenya hauwezi kusahaulika, sio mchache iImani yake isiyoyumba katika uwezo wa wachezaji chipukizi kutoka eneo la Mathare ambayo ilimwezesha kuwapa vijana wengi nafasi ya kuonyesha vipaji vyao vya soka. Chini ya uongozi wake wenye maono, Mathare United iliibuka imara na stadi katika soka la Kenya.

Chini ya usimamizi wake ambapo timu hiyo ilishinda taji la la Moi Golden Cup mnamo 1998, na kuwalaza AFC Leopards katika fainali ya kihistoria katika Uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Moi Kasarani.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kumbukumbu za aliyekuwa nahodha Francis Kimanzi akinyanyua kombe hilo la dhahabu na kusherehekea pamoja na maelfu ya mashabiki kutoka Mathare zitasalia katika kumbukumbu zetu milele. Ushindi haukuimarisha tu sifa ya klabu ya Mathare United bali pia uliwapatia matumaini makubwa vijana wadogo ambao kwa wakati huo hawakuwa na mbele wala nyuma.

Urithi wa Bob Munro umeandikwa sio tu katika mataji lakini katika taaluma ya baadhi ya wanasoka wakubwa wa Kenya.

Kupitia mikono yake, wachezaji kama vile Dennis Oliech, Titus Mulama, Salim Ali, Anthony Kimani,Matthew Ottamax, Duncan Ochieng, Simon Mulama, Asman Ngaywa, Walter Odede, Francis Ochieng, James Saruni, Jesse Were, Wyillis Oburu, Kepha Aswani, Jamal. Mohamed, Arnold Origi na maelfu wengine walipewa nafasi ya kutumia vipaji vyao kupitia kandanda.

Kuna wengi ambao walienda na kupeperusha bendera ya nchi hii katika viwango tofauti vya kimataifa. Mchango wake Munro haukuwa tu kuhusu kuendeleza wanasoka bali kuhusu kuchagiza maisha, kutoa matumaini, na kutengeneza njia ambazo hazikuwepo hapo awali katika eneo la Mathare na viunga vyake.

Maono ya Bob Munro yalienea zaidi ya soka. Kazi yake imeathiri vijana wengi huko Mathare na kwingineko, na kuwatia moyo kuwa na ndoto kubwa na kufanya kazi kwa bidii zaidi.

Alionyesha kwamba haijalishi asili ya mtu, kwa usaidizi na mwongozo ufaao, anga ndiyo kikomo.

Tunapomuaga Bob, tunasherehekea maisha yake, kujitolea kwake, na mchango wake kubwa katika mchezo wa kandanda nchini Kenya.

Umaarufui wake utaendelea kutia moyo vizazi vijavyo, na Mathare United itasimama milele kama ushahidi wa bidii yake, ari na kujitolea kwake kuinua soka ya Kenya.

Pumzika kwa amani, Bob Munro. Michango yako haitasahaulika, na urithi wako utaendelea kuwepo kupitia wachezaji na jumuiya ulizosaidia kuunda.