MTANGAZAJI nguli katika kuongoza vipindi vya miziki ya Reggae, Tallia Oyando maarufu kama Night Nurse ametangaza kufunga ukurasa wa safari yake ya utangazaji na runinga ya Citizen.


Kupitia chapisho la kipekee kwenye ukurasa wake wa Facebook alasiri ya Jumatatu, Oyando alisema kwamba miaka 8 katika kituo hicho cha runinga chini mwavuli wa Royal Media imemtosha na sasa ni muda wa kufungua ukurasa mwingine.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Aliwashukuru mashabiki wake wa kipindi cha Reggae, ‘One Love’ na kusema kwamba kuondoka kwake si kwaheri bali ni mapumziko ya muda kabla ya kuibuka tena.


“Baada ya miaka 8 maridadi ya mapenzi, muziki, na familia kwenye One Love katika Citizen TV, ni wakati wa sura mpya. Asante kwa kila mmoja wenu ambaye alifanya safari hii isiyosahaulika. Kama Joseph Hill alivyosema, 'Upendo hung'aa zaidi kuliko jua la asubuhi.' Hii sio kwaheri, mambo makubwa yanakuja. Tukutane kwa kipindi cha mwisho cha @onelovectv kwenye @citizentvkenya Jumamosi hii One Love, daima na milele,” Oyando alisema.


Mrembo huyo aliwaacha mashabiki wake na ujumbe kutoka kwa wimbo maarufu wa Redemption Song kutoka kwa gwiji wa utunzi wa miziki ya Reggae aliyewahi kuishi, Bob Marley.


“Ninapowaaga, ninawaacha na huu ujumbe wa kujikomboa kutoka kwa umaskini wa kifikira, hakuna mwingine bali ni sisi tunaoweza kujikomboa. Acha muziki uendelee kuzikomboa roho zenu, kuinua mioyo yenu na kutuunganisha sisi sote. Hii si kwaheri, ni kusherehekea muziki, kumbukumbu na ufamilia tuliounda pamoja. Kama nyimbo ambazo tulizienzi pamoja, upendo wangu kwenu hautayeyuka,” Oyando aliongeza.


Oyando alianza kuongoza kipindi hicho cha kila usiku wa Jumamosi kwenye runinga ya Citizen mnamo Oktoba 22, 2016 ambapo alikuwa akishirikiana na Coco Soboo Moto.