MSANII BIEN Aime Baraza ndiye mtumbuizaji mkuu atayaeongoza kundi la watumbuizaji wengine katika kuwaburudisha watu kwenye hafla ya kufanyika kwa droo ya michuano ya CHAN 2025.
Droo hiyo itafanyika usiku wa leo Jumatano Januari 15 katika ukumbi wa KICC kuanzia saa mbili usiku.
CAF kupitia tovuti yao wamethibitisha kwamba Bien ndiye mtumbuizaji mkuu atakayeburudisha wageni na washikadau wa michezo kwenye hafla hiyo.
“Matumbuizo manne mahiri ya muziki yatapanda jukwaani, yakitoa ladha ya urithi tajiri wa muziki wa kanda. Akiongoza burudani hiyo atakuwa Bien-Aimé Baraza, mwanachama wa kundi maarufu la muziki la Sauti Sol.”
“Bien atawaonyesha watazamaji baadhi ya nyimbo zake bora zaidi, zikiwemo Kuliko Jana—ushirikiano na Kwaya ya Red Fourth—pamoja na matoleo yake mapya zaidi Nairobi na Extra Pressure inayoongoza chati,’ CAF walithibitisha.
Pia watakaopamba jukwaa ni kikundi cha densi cha Uganda, Ghetto Kids, kinachojulikana kwa maonyesho yao yenye nguvu ya juu duniani kote.
Kujiunga nao kutakuwa na Kwaya ya Red Fourth ya Kenya, pamoja na kikundi cha densi cha kisasa, wakiahidi onyesho la kusisimua na tofauti.
Shabiki wa soka mwenye shauku na mfuasi wa AFC Leopards, Bien alionyesha furaha yake kuhusu kutumbuiza katika hafla hiyo ya kifahari.
"Nilipokua, nimekuwa shabiki wa mpira wa miguu barani Afrika. Kandanda na muziki vimeunganisha bara hili kama kitu kingine, na ni heshima kwangu kuungana katika hafla hii ya ajabu. Kuwa sehemu ya familia ya CAF kwa hili tukio ni ndoto kutimia," alinukuliwa na CAF.
Droo hiyo itafanyika siku moja tu baada ya CAF kutoa taarifa za kuahirishwa kwa michuano hiyo kutoka Februari hadi Agosti mwaka huu.
Hata hivyo, CAF haikubainisha tarehe kamili ya kufanyika kwa michuano hiyo mwezi Agosti na kusema kwamba taarifa hizo zitatolewa baadae.
CHAN, michuano inayoshirikisha wachezaji wa ligi za ndani pekee ilifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2009 nchini Ivory Coast.
Dhima ilikuwa kuboresha na kukuza ligi na wachezaji wa nyumbani. Makala ya mwaka huu yanaandaliwa kikoa baina ya mataifa matatu ya Afrika Mashariki – Kenya, Uganda na Tanzania.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!