MFANYIBIASHARA na mwanaharakati wa kisiasa, Morara Kebaso amefichua sababu iliyomfanya kupiga breki zoezi lake la kuchangisha pesa kwa ajili ya harakati zake za kisiasa kwenye mitandao ya kijamii.
Kupitia sasisho refu alilochapisha kwenye ukurasa wake wa X, Kebaso alifichua kwamba aliamua kusitisha kwa muda kuomba hela mtandaoni kwa vile alihisi watu wengi hawajaelewa maana ya kuchangisha.
Kebaso alisema kwamba aliamua kuwapa watu muda kupata uelewa kuhusu umuhimu wa kutoa michango ya kuendeleza kampeni.
“Kwa wale wanaoniuliza kwa nini tuliacha kukusanya fedha jibu ni rahisi. Tulihisi hatukuwapa watu muda wa kutosha kuelewa ni kwa nini tulihitaji kuchangisha pesa. Tulihitaji kuwapa watu muda wa kukuza uaminifu,” Kebaso alisema.
Mwanaharakati huyo hata hivyo alifichua kwamba hiyo haimaanishi ameacha kabisa kuchangisha pesa mtandaoni, kwani hivi karibuni ataanza tena baada ya watu kuelewa dhima ya michango hiyo.
“Kwa wale wanaouliza kama tutachangisha fedha siku zijazo jibu ni ndiyo tutafanya. Wakati huu itakuwa tofauti. Tumejifunza kutokana na makosa yetu,” Kebaso alisema.
Mwanachama huyo wa chama cha INJECT alisema umuhimu wa watu kuchangia harakati za siasa ni kwamba unapunguza ufisadi kwani watu wananunua sera na maono ya mwanasiasa.
Alisema kwamba bila mgombea kutumia pesa zake katika kampeni, inamzuia kutorudisha hela hizo baada ya kuchaguliwa kupitia kuiba mali ya umma.
“Iwapo mtu yeyote atatumia pesa zake kwa manufaa ya umma katika siasa, hakikisha atataka kuzirejesha. Ndivyo ufisadi unavyoanza. Ni bora kuchangisha jinsi inavyofanyika katika nchi zilizoendelea ili watu wakumiliki wewe na maono yako. Pia humsaidia kiongozi kubaki huru na asiwe mateka wa maslahi binafs,” Kebaso alisema.
Alitetea harakati zake za kuchangisha pesa mtandaoni akisema kwamba siasa ni ghali sana ikiwa mtu atatumia pesa zake mwenyewe.
‘Kwa wale wanaoniuliza kwa nini tulikuwa tunachangisha fedha kwa ajili ya shughuli za kisiasa jibu ni rahisi: siasa ni ghali sana,’ Kebaso aliongeza.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!