MSANII wa injili kutoka Tanzania, Rehema Simfukwe, amewaliza wengi baada ya kusimulia changamoto ambazo amepitia kwa kipindi cha miaka 6 akimlea mwanawe mwenye ugonjwa wa utindio wa ubongo (cerebral Palsy).
Akizungumza Jumapili katika hafla ya kuzindua kituo cha kulea watoto wenye tatizo hilo ambacho alijenga kwa ushirikiano wa mumewe, Simfukwe alisema kwamba hakuamini angekuwa mzazi mwenye mtoto wa tatizo hilo.
Mama huyo alifunguka kwamba baada ya kugundua mwanawe anaugua utindio wa ubongo (cerebral palsy) aliumia sana kiasi kwamba aliapa kutozaa tena.
“Nilipofahamu kuwa mtoto wangu ana utindio wa Ubongo (cerebral palsy) niliumia saaaana na kikubwa niliwaza kuwa future ya mtoto wangu itakuwaje?”
“Nilikuwa nakataa nasema hapana mtoto wangu ni mzima. Kulikuwa na changamoto nyingi ilifika wakati nikaapa kuwa sitazaa tena lakini Mungu aliinua watu wa kutusaidia na kutubeba yaani baba yangu na mama yangu na hii ilifika nguvu ya kuendelea hata nikapata watoto wengine yaani Deborah na Divine," Simfukwe alieleza baina ya kwikwi.
Alisema kwamba miaka 6 iliyopita, maisha yake yamekuwa magumu sana licha ya kuweka tabasamu mbele ya halaiki.
Msanii huyo alifichua kwamba wimbo wake pendwa wa “Chanzo” aliutunga baada ya madaktari kumfahamisha kwamba mwanawe anaugua cerebral palsy.
“'Chanzo' watu wengi walikuwa wakiniuliza
kwanini niliuandika. Na mara zote nilikuwa nikijibu kuwa wakati ukifika
nitasema na hatimaye wakati umefika…”
“Wimbo huu niliuandika nilipofahamu kuwa mtoto
wangu wa kwanza anaitwa Dorcas kuwa hatakuwa sawa na watoto wengine yaani ana
utindio wa ubongo. Mimi kama mama ilikuwa ngumu kwangu kukubali na kulipokea
hili maana wamama wanaelewa si rahisi kupokea jambo kama hili,” alisimulia.
Simfukwe alitambua na kushukuru juhudi za mumewe, Isaya Lyimo ambaye alisimama naye kwa ujasiri mkubwa pindi walipofahamishwa kwamba mwanawe hatakuwa kama watoto wengine.
Lyimo kwa upande wake alifichua kwamba alilazimika kuacha kazi aliyekuwa akifanya serikalini ili kusimama na mkewe katika malezi ya mwanao mwenye changamoto.
"Nilikuwa nafanya kazi serikalini na nikawa naomba uhamisho ili nirudi nishirikiane na mke wangu kulea mtoto na uhamisho ukawa unachelewa ikabidi niache nirudi nyumbani kumsaidia mke wangu.Mara nyingi mtoto hali inakuwa mbaya mke wangu akiwa kwenye huduma lakini nyakati zote Mungu amekuwa akitusaidia na ametupa watu wanatusaidia tunatoka kwenye huduma na kwenda hospitali," alisema.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!