MTANGAZAJI nguli wa kipindi cha Reggae katika stesheni ya Radio Jambo, Lion Deh ametupwa kwenye dimbwi la maomboleza kufuatia kifo cha mwanawe, Lion Jr.


Taarifa hizo za msiba zilifichuliwa na mtangazaji mwenza, Massawe Japanni JUmanne mchana alipowaarifu mashabiki wa Jambo kwamba Lion – ambaye hushirikiana na Mbusii Deh kuendesha kipindi cha Reggae kuanzia alasiri hadi usiku, asingeweza kutokea kwenye kipindi hicho.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Japanni alisema kwamba Lion anaomboleza kifo cha mwanawe ambaye amekuwa hospitalini kwa siku kadhaa hadi kifo chake.


“Lion Deh hataweza kuhudhuria shoo yao kwa sababu amefiwa na mtoto wake. Mbusii anaweza au asiweze pia kuwepo kwani wawili hao ni kama ndugu. Siwezi hata kufikiria jinsi ilivyo ngumu kupoteza mtoto, kama mama ninatuma rambirambi zangu,” Massawe Japanni alisema kwa sehemu katika kipindi chake cha Bustani.


Baadae, chanzo kilituarifu kwamba mwanawe Lion, ambaye ni wa chini ya mwaka mmoja alifariki baada ya kuanguka kutoka kwenye kiti sebuleni na kupata majeraha mabaya ya kichwa.


Majeraha hayo yaliathiri kwa kiasi kikubwa ubongo wa mtoto huyo, kumpelekea kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi kwa siku ayami.


Kwa mujibu wa mtaalamu wa afya, majeraha ya ubongo husababishwa mtu anapoangukia kichwa au kugongwa kwa kifaa butu kichwani.


Uharibifu wa ubongo baada ya kuanguka unaweza kusababishwa na jeraha la kiwewe la ubongo (TBI), ambalo ni neno pana kwa majeraha ya ubongo ambayo hutokea wakati nguvu ya nje inaathiri kichwa au mwili.


Kuanguka ni sababu ya pili kuu ya vifo vinavyohusiana na TBI, na ni kawaida kwa watu wazima na watoto wadogo.


Sababu nyingine ni pamoja na kugongana kwa magari, vurugu, na ugonjwa wa kutikisika kwa watoto.


Ukali wa TBI unaweza kuanzia mshtuko mdogo hadi jeraha kali ambalo husababisha kukosa fahamu au kifo.


Ukali huamuliwa na mambo mengi, ikiwa ni pamoja na asili ya jeraha, nguvu ya athari, na urefu wa muda ambao mtu hana fahamu.