Bi Caroline Mutai, mamake mchoraji katuni Gideon Kibet almaarufu Kibet Bull mnamo Jumatatu alithibitisha kuachiliwa kwa mwanawe na wanaodaiwa kumteka nyara.

Akizungumza na vyombo vya habari, Bi Mutai alisema kuwa mwanawe aliwasiliana naye mwendo wa saa nne alfajiri na kujitambulisha akisema alikuwa safarini akirudi nyumbani.

"Sahizi tumefurahi, tumewika. Aliniambia yuko Nakuru," Bi Mutai alisema.

Mamake Kibet alibainisha kuwa msimu wa sikukuu uliopita haukuwa wakati wa furaha kwake kwani alisikitishwa na kutoweka kwa wanawe wawili.

"Nililia; familia nyingine zilipokuwa zikifanya sherehe, nilikuwa nikilia nikisoma Biblia."

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Bi Mutai aliahidi kufanya karamu ya kusherehekea wanawe wawili, ambao walikuwa wametoweka na wamerejea nyumbani.

Kaka mdogo wa Kibet, Rony Kibet pia alipatikana akiwa hai Jumatatu asubuhi katika eneo la Machakos.

Kibet Bull alithibitisha kuachiliwa kwake Jumatatu jioni na kuweka wazi kuwa yuko salama na yuko sawa.

Akizungumza na waandishi wa habari, kijana huyo ambaye ni miongoni mwa wakosoaji kadhaa wa serikali waliodaiwa kutekwa nyara siku kadhaa zilizopita alifichua kuwa alitupwa katika kaunti ya Vihiga usiku wa kuamkia Jumatatu kabla ya kutafuta namna ya kufika nyumbani.

"Nilikuwa nataka nithibitishie Wakenya kwamba niko salama na nimefika nyumbani salama," Kibet Bull alisema.

“Mbeleni sikuwa najua niko wapi. Kidogo kidogo nilienda mbele niko Luanda, hapo Luanda nikatafuta mahali pa kukaa juu ya usalama mpaka ifike asubuhi ili nisafiri nyumbani. Niliachiliwa kitu saa tisa hadi saa kumi asubuhi,” niliongea.

Mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Egerton pia alifichua kuwa yuko vizuri kiafya na hana majeraha yoyote mwilini mwake baada ya kukaa siku nyingi na watekaji nyara wake. Pia alithibitisha kuwa kaka yake ambaye pia alidaiwa kutekwa nyara yuko sawa pia.

Kibet alitoa shukurani zake kwa wanamtandao wote walioshinikiza kuachiliwa kwao na kuendelea kuikosoa serikali kwa jinsi ambavyo imekuwa ikiwashughulikia wakosoaji.

“Kutekwa nyara kupo, naweza kuthibitisha hilo. Mimi naomba serikali kuwa na uhuru wa kuongea ama watumie kutumia poa kama kupeleka mtu kortini,” alisema.

Kibet alisema atakuwa akisimulia zaidi kuhusu mambo yaliyojiri na mipango yake ijayo baada ya akili yake kutulia.