Seneta wa kuteuliwa Crystal Asige ametoa ombi maalum kuhusu jambo ambalo hataki lifanyike wakati wa mazishi yake baada ya kufariki.

Katika chapisho la Jumamosi, mwimbaji huyo wa zamani katika Sol Generation aliomba wanasiasa wasiruhusiwe kuzungumza kwenye mazishi yake.

Seneta huyo alibainisha kuwa alikerwa na matukio yaliyojiri wakati wa mazishi ya mamake spika Moses Wetangula na mbunge Tim Wanyonyi katika kaunti ya Bungoma siku ya Ijumaa.

“Nitakapokufa, tafadhali- maikrofoni isipewe wanasiasa wowote kwenye mazishi yangu kwa sababu niliyosikia katika Kaunti ya Bungoma? Ulimwengu wote ni jukwaa marafiki zangu,” Crystal Asige aliandika kwenye Twitter.

Mwanasiasa huyo anayewakilisha watu wanaoishi na ulemavu katika seneti alitoa kauli hiyo siku moja tu baada ya mamake Wetangula na Wanyonyi, Mama Anne Nanyama, kuzikwa katika mazishi ambayo yalishuhudia wanasiasa wakishambuliana kwa maneno.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Majibizano ya maneno makali yalizuka kwenye mazishi hayo huku viongozi wakizozana kutokana na visa vya utekaji nyara vinavyoongezeka.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah alishindwa kujizuia na kumkemea gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kuhusiana na matamshi yake kuhusu utekaji nyara na mauaji ya watu ya kiholela.

Shambulio hilo lilijiri baada ya Natembeya kutokubaliana na matamshi ya Boss wa Cotu Francis Atwoli kuhusu utekaji nyara.

“Wewe ni afisa; ikiwa unajua watu wanatekwa nyara, shiriki taarifa na polisi lakini usije hapa kumfokea Atwoli (bosi wa COTU),” Ichungwa alisema.

Ichung’wah alibainisha zaidi kuwa Natembeya alikuwa mkuu wa mkoa katika utawala uliopita, ambao pia ulishutumiwa kwa utekaji nyara na mauaji ya nje ya mahakama. Ichung’wah baadaye aliomba msamaha kwa waombolezaji na familia iliyofiwa kwa jinsi alivyojibu matamshi ya Natembeya.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja Rais William Ruto, Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Musalia Mudavadi, mkuu wa COTU Francis Atwoli, magavana Ken Lusaka (Bungoma) na Paul Otuoma (Busia), Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohammed mtawalia na kundi la wabunge na maseneta.