MWANASOSHOLAITI Zari Hassan amekuwa mtu mashuhuri wa hivi punde kuguswa na msiba wa mwanasoka Ezekiel Otuoma.


Mkewe Rachael Otuoma alitangaza kifo hicho alfajiri ya Jumamosi ya Desemba 21 kupitia kurasa zake za mitandaoni na kuwaacha mashabiki wao wengi katika hali ya huzuni.


Ezekiel Otuoma amepumzika baada ya vita vya muda mrefu na Motor Neuron Disease. Ugonjwa wa Motor neurone, ni hali ambayo huathiri neva, husababisha udhaifu katika misuli, na kusababisha hatimaye kupooza. Aligunduliwa na ugonjwa huo mnamo 2020.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Zari kupitia ukurasa wake wa Instagram, alisema kwamba japo hakuwa anamjua Otuoma moja kwa moja lakini kifo chake kilimgusa.


Mama huyo wa watoto watano Mganda mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini alisema kwamba alipata taarifa za kifo cha Otuoma kupitia TikTok ambapo Rachael na Otuoma walikuwa na ufuasi mkubwa.


“Ni siku nyingine tena ya kulia na watu nisiowajua. Moyo wangu unatokwa na damu, nilipata taarifa za kifo cha Otuoma kupitia TikTok. Pumzika kwa Amani shujaa, na ninakuombea wewe Rachael,” Zari Hassan aliandika.


Mpenzi huyo wa zamani wa mwanamuziki Diamond Platnumz alimpa heko na hongera za dhati, Rachael Otuoma kwa kusimama na mumewe muda wote alipokuwa hawezi kujifanyia kitu chochote, hadi siku yake ya mwisho duniani.


Zari alisifia mapenzi ya dhati ya Rachael kwa mumewe, kwa kuwa na uvumilivu wa kumhudumia kwa zaidi ya miaka 3 akiwa anatumia kiti cha magurudumu.


“Mapenzi kama haya!” Zari aliandika katika picha nyingine ya Rachael na Otuoma akiwa kwenye kiti cha magurudumu na Rachael alimchangamsha kwa kumchezea ngoma na ndensi taratibu.


Otuoma atakumbukwa katika historia ya Soka ya Kenya akiwa amechezea Vilabu maarufu kama AFC Leopards, Western Stima, Ushuru miongoni mwa vilabu vingine ambapo alikuwa winga matata.