MFANYIBIASHARA Gibson Murage Gitonga wa Modern Furniture Pacific ametoa taarifa njema kwa wafanyikazi wake wa kiwanda cha Ruiru waliobaki kwenye njia panda baada ya moto kuteketeza kiwanda hicho cha kuuza fenicha wiki jana.


Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Gibson Murage alitangaza kwamba tukio la wiki jana katika tawi la Ruiru lilikuwa la kuhuzunisha na lisilotarajiwa lakini lilimsukuma kutafuta mbinu mpya ya kuendeleza biashara yake.


Mjasiriamali huyo alifichua kwamba tayari amenunua vyomvo vipya vya kazi ili kuchukua nafasi ya vile vilivyochomeka wakati wa mkasa huo.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Murage alisema kiwanda hicho kitarejelea shughuli zake ifikapo Jumatatu, na kufichua alichukua hatua hiyo ili wafanyikazi wanaotegemea kazi hiyo wasije wakaenda nyumbani kwa kupoteza kazi.


“Baada ya ajali ya moto isiyotarajiwa, nililazimika kuwa na mpango mpya. Kufikia leo, tuna vifaa vipya katika kituo chetu cha uzalishaji. Uwe na uhakika kwamba kufikia Jumatatu asubuhi, kila kitu kitakuwa kinaendelea vizuri.”


“Ilitubidi kufanyia kazi hili ili hata mamia ya wafanyikazi wanaotegemea Modern Furniture Pacific wasirudi nyumbani. Nimefurahi sana kwamba watarudi kazini. Niliwaahidi kuwa Kazi zao ziko salama.”


“Asante kwa usaidizi wako wa ajabu na ujumbe wa faraja. Sasa tumerudi ili kuendelea kupiga mbao kwa mtindo wako,” Gibson Murage alisema akionyesha baadhi ya vifaa vipya alivyovinunua.


Murage aliwashukuru baadhi ya watu ambao wamekuwa wakifanya kazi naye katika kutangaza biashara yake, akifichua kwamba mmoja wa mabalozi wake wa matangazo ya biashara, Dem wa Facebook alimtembelea ofisini.


“Nimebarikiwa sana kuwa na watu fulani maishani mwangu. Asante kwa kufanya maisha kuwa ya kufurahisha zaidi na moyo wangu kuwa mwepesi kidogo. Ni baraka kuwa na watu ambao hawakati tamaa juu yako na wanaokuinua kila wakati unapokuwa chini. Bwana Mwenyezi Mungu aendelee kukubariki. Familia ya Modern Furniture Pacific ina furaha kwa ajili yako DEM WA FB,” Murage alimshukuru mrembo huyo.


Katikati mwa juma lililopita, mashabiki wa Murage walimhurumia baada ya picha kuenezwa zikimuonesha akiwa amezubaa bila kuamini macho yake jinsi duka lake la Ruiru lilikuwa limemezwa katika moshi mkubwa.