WAKILI Ahmednasir Abdullahi ameomba msamaha wa dhati
kwa mashabiki wa klabu ya ligi kuu Uingereza, Arsenal baada ya kuitaka klabu
hiyo kumsaini mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford.
Siku chache zilizopita baada ya Rashford kutangaza kwamba anahisi muda umefika kujaribu changamoto mpya mbali na Man Utd, Ahmednasir alishauri kwamba huu ndio wakati mwafaka kwa Arsenal kuchangamkia fursa hiyo.
Ahmednasir, shabiki kindakindaki wa Arsenal alisema kwamba Arsenal wanafaa kuchukua fursa hiyo kwa haraka na kumleta Rashford ugani Emirates.
“Arsenal wanapaswa kumnunua Rashford katika dirisha la usajili la Januari,” Ahmednasir aliandika kupitia ukurasa wake wa jukwaa la X.
Hata hivyo, alipokea maoni kinzani kutoka kwa mashabiki wenzake jambo lililompelekea kufanya tathmini ya kina na kuibuka na mtazamo mpya kuhusu Muingereza huyo mwenye umri wa miaka 27.
Wakili huyo alibaini kwamba Rashford huenda asiwe wa umuhimu wa kipekee kwa Arsenal baada ya kupitia takwimu za uchezaji wake katika klabu ya Man Utd.
Alifikia uamuzi kwamba Rashford ni mchezaji wa kawaida tu kama wengine ambaye hawezi akaisaidia Arsenal katika mbio zao za kusaka ubingwa wa EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20.
Alitangaza kuomba msamaha mashabiki wenzake wa Arsenal na kuondoa kauli hiyo ya kumtaka Rashford Arsenal.
“Misimu 10, mechi 439, mabao 139. Samahani, hiyo ni wastani sana. Ninaondoa kwa kuomba msamaha, pendekezo langu,” Ahmednasir alisema.
Rashford amehusishwa kuondoka Man Utd haswa baada ya kuachwa nje ya kikosi kilichomenyana na watani wao wa jadi Manchester City wikendi iliyopita.
Hata hivyo, licha ya kumuacha nje ya kikosi, kocha mkuu Ruben Amorim anasisitiza kwamba Rashford bado ni mchezaji wa Man Utd na asingependa aondoke.
'Klabu ya aina hii inahitaji talanta kubwa na ana talanta kubwa, kwa hivyo anahitaji tu kufanya kiwango cha juu na hiyo ndiyo umakini wangu. Ninataka tu kumsaidia Marcus.
‘Hakuna kilichobadilika. Tunamwamini Marcus. Marcus ni mchezaji wa Manchester United, kwa hiyo hakuna mabadiliko.’
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!