MSANII wa kizazi kipya nchini Kenya, Willy Paul
amefichua kwamba kipindi cha wiki moja iliyopita kimekuwa kipindi cha mavuno
makubwa kwa upande wake.
Pozee ambaye amekuwa midomoni mwa watu wengi tangu usiku wa Desemba 7 wakati wa mfarakano ulioshuhudiwa katika tamasha la Furaha Fest jijini Nairobi, amefichua kwamba akaunti zake za mitandao ya kijamii zimeshiba pakubwa kwa kipindi hicho.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Willy Paul alifichua kwamba amepata wafuasi wapya zaidi ya laki moja kwenye TikTok na wengine wapya zaidi ya laki na nusu kwenye chaneli ya YouTube.
Msanii huyo zamani akiwa wa injili hakusita kutambua kwamba hizo kwa asilimia kubwa ni juudi za mashabiki wake wa Kenya.
“Wakenya Wamefanya. Tik Tok Yangu Imepata Wafuasi 100k Zaidi, YouTube Yangu Imevutia Wafuatiliaji 150k Zaidi,” Willy Paul alifichua.
Willy Paul baada ya kufarakana na usimamizi wa Diamond Platnumz katika tamasha la Furaha Fest lililoandaliwa katika Polo Club, amekuwa katika mstari wa mbele kudai kwamba ndiye mpiganaji mkuu wa haki sawa kati ya wasanii wa Kenya na wasanii wa kigeni.
Msanii huyo alidaiwa kuzushiana vurugu baada ya ratiba ya kutumbuiza kwake kubadilishwa kinyemela, vurugu ambazo zilimfanya Diamond kutopata nafasi ya kutumbuiza katika usiku huo wa tafrija.
Hata hivyo, baadae katika taarifa yake kwa njia ya video, Diamond alikanusha kwamba kutotumbuiza kwake hakukuwa na uhusiano wowote na Willy Paul bali ni wasimamizi walifeli katika kuhakikisha kuna utulivu.
Msanii huyo wa Bongo alifichua kwamba alilipwa zaidi ya shilingi milioni 19 za Kenya na kudokeza kwamba asingerudisha hata senti baada ya kutotumbuiza, kwani waandalizi ndio walienda kinyume na maagano ya mkataba wa ujio wake.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!