
Mahakama kuu mjini Eldoret imemhukumu mpiga picha wa kujitegemea Jacktonne Odhiambo, almaarufu Lizer, kutumikia kifungo cha miaka 50 kwa mauaji ya mwanaharakati wa LQBTQ Edwin Kiptoo Chiloba mjini Eldoret.
Jaji Reuben Nyakundi alitaja mauaji hayo kuwa yaliyopangwa na kutekelezwa kikatili. Alisema mshitakiwa haonyeshi majuto ya dhati tangu alipotekeleza mauaji hayo na alistahili adhabu ya kifo.
Nyakundi alisema ushahidi katika kesi hiyo ulipendelea maombi ya hukumu ya kifo. "Nimeliangalia suala hili na kupima mizani yote. Utatumikia kifungo cha miaka 50 jela kwa kosa hili", alisema Nyakundi.
Hakimu alisema aina na namna ya kumuua marehemu ilikuwa ya kinyama kwa sababu mshtakiwa aliingiza jozi sita za soksi kooni na kunyima oksijeni na kusababisha kuharibika kwa mfumo wa mwili wa marehemu.
"Mauaji hayo yalipangwa kwa nia mbaya na nia mbaya kiasi kwamba mshitakiwa alitumia fedha kwa ajili ya marehemu kununua boksi la chuma, kukodi gari la kubebea maiti na kuficha ushahidi" , alisema Nyakundi.
Kabla ya hukumu hiyo, Gaudensia Chelimo ambaye alikuwa binamu wa marehemu aliiomba mahakama hiyo hukumu ya kifo au kifungo cha maisha jela.
"Labda hiyo itaifurahisha familia ingawa haitamrudisha kaka yetu", alisema huku akilia kortini. Alisema familia ilisononeka kwa sababu Chiloba alikuwa mtoto wa kiume pekee katika familia yake ambaye alikuwa na mustakabali mzuri.
"Alimuua mtoto wetu kwa kumwingiza kikatili jozi tatu za soksi mdomoni ilhali walikuwa marafiki", alisema Gaudensia.
Alisema marehemu alikuwa mtoto wa pekee kwa baba yake na alifariki kabla ya kuzaa na hivyo kizazi kizima katika ukoo wake kilipotea kutokana na kifo hicho.
“Tulishangaa kumkuta kwenye chumba cha kuhifadhia maiti akiwaambia watu kuwa yeye ndiye ndugu pekee wa marehemu.
Hakuwa na haya na alitumia pesa zake kununua nguo na wanawake kwani mtoto wetu alikuwa akiozea kwenye chumba cha maiti,” alisema.
Wakili Mathai alisema mshtakiwa akiwa na umri wa miaka 25 alikuwa rumande kwa miaka miwili na alithibitisha kuwa aliweza kubadilika na kujumuika na jamii.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!