MSANII wa Kings Music, Alikiba ameonekana
kutofurahishwa na kauli ya msanii kutoka lebo pinzani ya WCB Wasafi, Mbosso
Khan kwamba yeye [Alikiba] amezeeka.
Mbosso na Alikiba walikuwa katika hafla ya kimuziki ya mwanasiasa mmoja eneo la Rufiji nchini Tanzania ambapo kila mmoja alitumbuiza kwa wakati wake.
Baada ya shoo, Mbosso alifanya mahojiano na waandishi wa Habari ambapo alimtaka Alikiba kuweka pembeni bifu na badala yake kumfuata Diamond Platnumz leboni Wasafi kwa ajili ya kolabo ya kumaliza uhasama.
Kwa mujibu wa Mbosso, Alikiba sasa hivi ameshakua mtu mzima na katika uzee wake, hafai kuendekeza bifu la kimuziki na Diamond.
Mbosso alisema kwamba yeye alishawahi kutembea katika lebo ya Kings Music na kukutana na Abdukiba, mdogo wake Alikiba.
Hivyo, alimtaka Alikiba pia kurudisha mkono kwa kutembea leboni WCB Wasafi na kumkuta Diamond ili wamalize uhasama.
“Alikiba ni vile hajaongea tu vizuri na mwamba yule [Diamond]. Angekuja kule angefanya tu kolabo. Anakaribishwa kule. Mimi nishawahi enda Kings Music, anatakiwa aje yeye sasa,” Mbosso alisema kwa sehemu.
“Eeh bwana mzee, unazeeka, hayo mambo hayatakiwi sasa hivi, njoo kule [WCB Wasafi] ufanye kolabo,” aliongeza.
Hata hivyo, Alikiba kwa kauli ya kutoridhishwa na kuitwa mzee, alisema kwamba yeye hana haja yoyote ya kuenda Wasafi kwani ujio wa Mbosso Kings Music haukuwa kwa ajili yake.
Alikiba alisema pengine Abdukiba ndiye tu anaweza kutembea Wasafi lakini si yeye.
“Kwa nini kwanza mimi niende Wasafi? Kwa sababu yeye alikuja kwa ajili ya Abdukiba inabidi tu Abdukiba yeye ndiye aende kule. Hakuna sababu ya mimi kunifanya niende kule not unless nataka kufanya kazi. Lakini sina kazi. Sina maana kwamba nashindwa kuenda lakini sina kazi ya kufanya,” Alikiba alijibu.
“Mimi sina sababu ya kushindana na zamani nilishawahi kutukanishwa hadi na mamangu matusi ya nguoni, wakaona hilo sijibu na sasa hivi wamekuja na kampeni nyingine kwamba nimeisha, sijui nimezeeka. Wanaosema nimezeeka, muda utasema na wakae wakijua kwamba uzee ni kifo,” alimaliza.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!