
Kocha mkuu wa AFC Leopards Mike Ambani alikuwa mwingi wa tabasamu, furaha na bashasha baada ya timu yake kulaza Tusker FC 4-1 katika mechi ya kuburudisha ya Ligi Kuu ya Kenya uwanjani Dandora Jumatano.
Ambani alisema kuwa ushindi huo mkubwa dhidi ya Watengenezaji Bia hao wa Ruaraka ni kielelezo cha bidii na ari ya timu hiyo.
Ochieng Ovella alipachika wavu sekunde chache kabla ya mapumziko, kisha Sydney Lokale, Victor Omune na Bonface Munyendo wakahakikishia Leopards ushindi na mabao mengine baadaye.
Ambani, akionekana kufurahishwa na uchezaji wa timu yake, aliwamiminia sifa tele, akiangazia nidhamu yao ya kimbinu na moyo wa kutoyumba.
"Tulitekeleza mpango wetu wa mchezo bila dosari, na kuzima mashambulizi ya Tusker huku tukitumia udhaifu wao wa Ulinzi kupata mabao," Ambani alisema.
Ambani alisema kupiga pasi sahihi, mwendo wa akili, na mfumo imara wa ulinzi, uliwawezesha kudhibiti kasi ya mchezo na kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.
"Zaidi ya hayo, kujitolea na dhamira isiyoyumba ya wachezaji ilijitokeza. Walionyesha njaa ya ushindi, wakisonga mbele bila kuchoka na kukataa kuzuiwa na majaribio ya Tusker ya kurejea," Ambani alisema.
Ambani alidokeza kwamba wachezaji wake Sana nguvu inayohitajika kuwania taji hilo. "Sasa tumejiweka katika nafasi nzuri ya kuwania taji hilo na tumejipanga kikamilifu kulihusu," alisema.
"Roho hii ya kutoyumba, pamoja na ustadi wao wa kiufundi, ilisababisha utendaji bora ambao haukuacha shaka juu ya uchezaji wetu," alisema.
Kipigo kikubwa cha Tusker FC kiliacha ladha chungu vinywani mwa mashabiki na wachezaji vile vile. Kocha mkuu wa Tusker Charles Okere alikosoa vikali uchezaji wa timu yake.
“Kuchanganyikiwa kwangu kunaeleweka, mpango wetu haujafanikiwa leo, tulipanga kuanza mchezo kwa kasi kubwa lakini tukaishia kuanza kwa ulegevu. ili tupate nafuu,” alisema.
Alisema analenga kuweka hali ya dharura na uwajibikaji ndani ya kikosi hicho. "Tunatumai kuwa wachezaji wamekusanya mafunzo muhimu kutoka kwa mchezo na kupoteza kutatupa motisha ya kufanya kazi kwa bidii na kuboresha utendaji wetu katika mechi zijazo," alisema.
"Kipigo hicho hakikuwa tu pigo kwa ari yetu bali pia kikwazo kikubwa katika harakati zetu za kuwania ubingwa wa ligi," Okere alisema.
Kwingineko, mabingwa watetezi Gor Mahia walipoteza uongozi wa mapema na kushiriki viporo na Shabana katika pambano la kusisimua lililoisha 1-1.
Talanta iliishinda Mara Sugar mabao 2-0 huku Kenya Police ikiizaba Bidco mabao 3-0.
Kariobangi Sharks walitoka sare ya bila kufungana mawili dhidi ya Nairobi City Stars huku Ulinzi Stars na Bandari zikitoka sare ya 1-1.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!