MSANII kutoka lebo ya Konde Music Worldwide, Harmonize amekuwa wa hivi punde kuweka kwenye mizani suala la kufarakana kwa Willy Paul na Diamond kwenye steji wikendi iliyopita.


Harmonize, ambaye amekuwa akifuatilia zogo hilo kwa ukaribu japo kimya kimya, alisema kwamba kilichomkuta Diamond kikimtokea katika shoo yake nchini Uganda, kesi itaishia polisi.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Msanii huyo alitamba kwamba akitokea msanii yeyote wa kujaribu kuvuruga shoo yake inayotarajiwa kufanyika nchini Uganda mwishoni mwa mwaka, basi yeye hatokaa kutulia bali atamkabili msanii huyo kwa makofi na vibao, kisha shoo iendelee na baadae kesi isuluhishwe polisi.


Harmonize alisema hakuna msanii yeyote nchini Uganda atakayejaribu kuvuruga shoo yake au kuisitisha isipokuwa tu rais wa taifa hilo, Yoweri Museveni.


“Uganda ?? team no excuses coming ? kama kuna msani wenu mkorofi mkorofi mwambie ni kabisa atapigwa !!! Nakamata natia vibao!!! Show itafanyika kisha tutakutana polisi ? hakuna wakunizuia kuimba labda mwenyewe rais @kagutamuseveni mtu mwema sana ️ tukutane hapo bange,” Harmonize aliandika.


Kauli yake ilionekana kurejelea kilichotokea katika ukumbi wa Polo Club wakati wa Furaha Fest na kusababisha Diamond kuondoka bila kutumbuiza.


Uvumi wa awali ulidai kwamba Diamond na Willy Paul walivurugana kila mmoja akipambania muda wa kuingia kwenye steji.


Hata hivyo, Diamond katika taarifa yake kwa njia ya video alikanusha uvumi huo akisema kwamba yeye hangeweza kupigania kuingia stejini kwani tayari alikuwa ameshalipwa.


Msanii huyo alisema kuwa kilichosababisha yeye kutotumbuiza ni vurugu zilizokuwa zikiendelea kwenye ukumbi, akisema kuwa muda wote alisalia katika gari lake hadi meneja wake alipoamua kumrudisha hotelini.


Diamond alisema hakuna chochote alikipoteza kiasi cha kumtaka kupambania kuingia stejini, akisema tayari alikuwa amelipwa zaidi ya shilingi milioni 19.


Aliwalaumu waandaaji wa kuponza shoo kwani walishindwa kutuliza vurugu ili apate nafasi ya kuingia stejini kuwapa mashabiki burudani.


Alimtaja Willy Paul kama msanii aliyekuwa akijaribu kulivuta jina lake kwa matope ili akitafuta kiki, huku akisisitiza kwamba hakuna mahali walikutana na msanii uyo au kubishana kwani muda wote yeye alikuwa ndani ya gari lake.