MSANII wa kutoka humu nchini, Willy Paul amejitokeza
na kuzungumzia vitisho violivyorekodiwa na chawa wa Diamond Platnumz, Mwijaku
akimzomea kwamba hatomaliza mwaka huu na kuingia mwaka mpya salama.
Mwijaku, katika video ambayo imewagawanya watu mitandaoni, alimpa onyo kali Willy Paul akimtabiria kupatwa na jambo baya baada ya kuvurugana na Diamond wikendi iliyopita jijini Nairobi.
Mwijaku alimwambia Willy Paul kwamba kwa kumvuruga Diamond hadi kumfanya kuondoka Kenya bila kutumbuiza, alifanya kosa lisiloweza kusameheka.
Mbwatukaji huyo wa mitandaoni alifananisha kitendo cha Willy Paul kumvuruga Diamond kama mwanamume kuingia choo cha kike, akisema kwamba yatampata makubwa kabla mwaka huu kukamilika, zikiwa zimesalia takribani siku 20.
“Willy Paul, umeingia choo cha kike. Ukivuka huu mwaka kuingia 2025, labda mimi sio Mwijaku,” chawa huyo wa Diamond alisema.
Hata hivyo, Pozee alionekana kutoyumbishwa na kauli hiyo akisema kwamba bado azma lake ni kuendelea kupigania muziki wa Kenya, liwalo na liwe.
Pia alisema kwamba atavuka mwaka 2025 salama na ataendelea kuwepo hadi pale atakapoukomboa muziki wa Kenya kutoka mikononi mwa mabepari.
“Wasanii wa Kenya Wanastahili Heshima. Sasa hii ni nini? Hivyo kusimama Na Ukweli ni Wrong Just Because Mtu Ni Mkenya? Nitamaliza mwaka Hadi 2025 Na Miaka mingine Kwa Jina La Yesu. Kama nilivyosema, Nitapigania Nchi Yangu na Sekta ya Kenya Hadi Tupate Heshima Tunayostahili,” Willy Paul alisema.
Kuvurugana na Willy Paul kulikuwa moja ya tukio kubwa kutoka kwa Furaha Fest ambalo limekuwa likizungumziwa na watu kutoka matabaka mbalimbali nchini Kenya na Tanzania.
Uvumi wa awali ulidai kwamba Diamond na Willy Paul waliburuzana baada ya kutokea kutokuelewana kuhusu ni nani kati yao angefaa kutumbuiza wa kwanza.
Hata hivyo, Diamond aliondoka katika hafla hiyo kwa ghadhabu baada ya mashabiki kumfokea wakiimba jimba la Willy Paul.
Baadae, uongozi wake ulitoa taarifa ambapo walisema kuwa Diamond kukosa kutumbuiza haikuwa kwa sababu ya Willy Paul bali ni suala lililojiri baina yao na waandaaji wa hafla hiyo.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!