MKEREKETWA mkali wa siasa za chama cha ODM, Calvince Gaucho amekuwa mtu wa hivi punde kutoa maoni yake kuhusu zogo lililojiri baina ya wasanii Willy Paul na Diamond Platnumz wikendi iliyopita.


Mfarakano huo ulitokea ukumbini katika shoo ya Furaha Fest jijini Nairobi wakati walianza kubishana kuhusu ni nani anafaa kuwa wa kwanza kuingia jukwaani.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Gaucho alisema kwamba si vibaya kwa watu kumtetea wa kwao lakini akasema hilo linafaa tu kuwa humu nchini na wala si kuvuka mipaka, kwani linaweza likaathiri hata wafanyibiashara.


“Kuna kitu Wakenya tumeanza kufurahia haya mambo tulianza na Gen Z, tunasema leo hiki hakitufurahishi tukiache…ni kitu kizuri tukikifanya wakati mwingine sisi kwa sisi tu kama Wakenya. Lakini ikianza kuvuka mipaka, tutakuwa na shinda nyingine mbaya,” Gaucho alisema.


“Watu wengi wanaona hii vita ni kama ya Willy Paul tu na Diaqmond, hawajui inaweza enda mbali hadi ifike kwa wafanyibiashara ambao wanafanya pia biashara Tanzania,” Gaucho aliongeza.


Gaucho aliendelea na kumsuta Willy Paul kwa kumvuruga Diamond katika Furaha Fest, akisema kuwa muziki wa Kenya aliodai kupigania ulishakufa kitambo na enzi za Genge ya JuaCali na wenzake.


“Si vibaya kusapoti mtu wetu, lakini pia lazima tuambiane ukweli. Muziki wa Kenya uliisha na kina JuaCali. Hata kama walikuwa wanapiga genge lakini ilikuwa ni genge yenye ujumbe na hawakuwa wanakesha kwa mambo ya kiki, fitina na udaku,” Gaucho alisema.


Mwanasiasa huyo alisema kwamba kama Wasanii wa Kenya wanataka Wakenya waanze kusikiliza miziki yao, ni sharti wajitutumue zaidi kwa kufanya miziki yenye maana.


“Mimi kwangu niko na flash 6. Tatu ziko na miziki ya Jamaika, mbili ziko na miziki ya Tanzania na zingine kutoka Kongo na Uganda. Kwa sababu gani? Sasa mimi nianze kusikiliza miziki ya Bahati kwa sababu wanazunguka na Diana jikoni? Siwezi!”


“Wasanii wa Kenya kama wanataka tusikilize miziki yao, ni lazima wafanye muziki mzuri ambao uko na ujumbe,” Gaucho aliongeza.


Zogo la Willy Paul na Diamond wikendi iliyopita limezua mjadala mkali mitandaoni, Wakenya wakichukua misimamo tofauti kuhusu tukio hilo lililosababisha Diamond kutotumbuiza.