WABABE wa soka kutoka Misri, Al Ahly wamejitokeza
kunyoosha maelezo kuhusu tetesi zinazoenezwa mitandaoni kwamba wamo katika safu
ya vilabu vinavyowinda huduma za Cristiano Ronaldo.
Mreno huyo mwenye umri wa miaka 39 amekuwa akihusishwa na kuondoka Al Nassr ya Saudi Arabia mwishoni mwa msimu huu huku vilabu kadhaa vikitajwa kuwa katika mbio za kuwania saini yake.
Mkataba wa Ronaldo na Al Nassr unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa msimu na yupo huru kufanya mazungumzo ya kujiunga na klabu yoyote kuanzia mwezi Janauri iwapo Al Nassr hawatampa mkataba mpya.
Moja ya vilabu ambavyo vimetajwa wiki hii ni Al Ahly kutoka Misri ambao wamesemekana kuwa katika harakati za kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya michuano ya mwisho wa msimu – FIFA Club World Cup kati ya Juni na Julai mwakani.
Klabu hiyo kutoka Cairo iko katika kundi A na Inter Miami yake Lionel Messi, Porto, na Palmeiras.
Hata hivyo, uwezekano wa Ronaldo kuelekea Misri unabaki na nafasi finyu baada ya ripoti kutoka klabuni kuibuka kwamba Al Ahly hawako na mpango wa kumsajili Ronaldo.
Kwa mujibu wa Koora, chanzo kilicho karibu na uongozi wa klabu hiyo, Al Ahly hawako tayari kufukuzia saini ya Ronaldo kutokana na gharama kubwa ya mchezaji huyo maarufu kote duniani.
“Klabu yoyote itataka kumsajili Ronaldo kwa sababu ni nguli wa soka na maarufu katika hilo, lakini jina lake halikuwa miongoni mwa majina ambayo tuliwasilisha katika meza ya majadiliano ya Al Ahly kwa sababu maelezo ya mkataba na malipo ya mchezaji huyo yapo juu sana,’ chanzo kilisema.
“Ronaldo anapokea mshahara mkubwa na Al Nassr ambao ni mkubwa kuzidi bajeti nzima ya klabu ya Al Ahly,” ripoti hiyo iliongeza.
Ripoti hizi zinachipuka wakati ambapo kuna uvumi kwamba Ronaldo yuko tayari kushiriki katika michuano ya FIFA Club World Cup, baada ya klabu yake ya Al Nassr kufeli kujishikia nafasi.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!