Msanii wa Amapiano ya Kiswahili kutoka Tanzania, Chino Kidd ameahidi kumpa shavu rapa wa humu nchini Stevo Simple Boy.


Akizungumza katika mahojiano kwenye runinga ya TV47, Chino Kidd alisema kwamba angependa kumsaidia Stevo Simple kwa kutimiza moja ya ndoto zake ambayo ni kukutana na Diamond kwa ajili ya kolabo.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Chino Kidd alifafanua kwamba yeye yuko tayari kwa asilimia 100 kushirikiana na Stevo Simple Boy kwenye kolabo lakini pia kumpeleka moja kwa moja hadi kwa Diamond Platnumz.


Aliyasema hayo baada ya Dr Ofweneke kumuuliza kama anaweza kumsaidia Stevo Simple Boy, aliyempigia debe kama kijana mwenye talanta ambaye amejituma sana kimuziki.


“Mimi ninaweza fanya muziki na Stevo Simple Boy 100% na nitambeba pia nitaenda naye Tanzania na hata kumkutanisha na Diamond.   Lakini pia nitafanya naye interview kule kwa sababu watu wanamfahamu kule, mimi mwenyewe nilimjua na nikamfollow,” Chino Kidd alisema.


Hata hivyo, msanii huyo alisema kumkutanisha Stevo na Kajala ni nje ya uwezo wake kwa kile alichokitaja kuwa aliwahi kumsema vibaya Harmonize – ambaye bado anaonekana kuvutiwa na ex wake, Frida Kajala katika siku za hivi karibuni.


Iwapo Chino atafanikisha kumkutanisha Stevo na Diamond basi itakuwa ni ndogo iliyofaulu kwa msanii huyo ambaye miezi michache iliyopita alimtania Diamond kwamba angemtoza hela ndefu ili kufanikisha kolabo.


 "Diamond, ulinitumia meseji kwenye Instagram ukisema unataka collabo, lakini usipokohoa Sh20 milioni, hakuna dili,” Aliyejitangaza Mfalme wa Afrika, Stevo Simple Boy alisema.


 


Wiki mbili baadae, msanii huyo alilazimika kutetea uamuzi wake wa kudai milioni 20 ili kupata kolabo na Diamond.


 


 


Kulingana na Simple Boy, Wakenya wamechangia pakubwa mafanikio ya Diamond kimuziki.


 


“Ni kweli nilisema hivyo kwa sababu ukitutazama sisi Wakenya tumemuunga mkono Diamond mpaka amefikia, kwanini asirudishe mkono wake na kufanya kolabo na msanii wa Kenya? Steve alisema.


 


Msanii huyo pia alienda mbali zaidi na kufichua kuwa kauli hiyo iliwatia kiwewe Watanzania kiasi kwamba vyombo vingi vya habari kutoka nchini humo vilimtafuta kwa njia ya simu kumtaka aeleze zaidi.


 


“Vyombo vya habari vya Tanzania vilinipigia simu, vikisema Steve umefanya jambo la maana kwa sababu tunaona kazi yako Kenya, wakasema pia Diamond ana haki ya kutoa Sh20m hivyo nimpe ushirikiano,” alieleza.


Kwa mara kadhaa, msanii huyo wa Kenya amekuwa akijinadi kama Diamond wa Kenya.


“Najua Wakenya na watu wengine walikuwa wanasema eti mimi ni Diamond wa Kenya. Kwa hiyo mimi nilikuwa nasema hizo zikitulia naachilia ngoma, unaona.”