Bosi wa lebo ya Konde
Music Worlwide, Harmonize amezua sekeseke mitandaoni baada ya kudai kwamba yeye
ndiye msanii pekee kutoka Tanzania mwenye ubora katika kuandika na kuzungumza
lugha ya Kiingereza.
Msanii huyo alifichua hayo katika ukurasa wake wa Instagram, akisema kwamba anaamini hakuna msanii kutoka Tanzania anayempiku wala kumkaribia katika ubora wa kuandika na kuzungumza Kiingereza.
Msanii huyo aliongeza kuni katika madai yake akisema kwamba tangu ujio wa muziki wa Bongo Fleva miaka ya 90, hakuna msanii aliyefanya uthubutu wa kuimba katika Kiingereza na wimbo ukawa mkubwa.
‘Tangu Bongo Fleva ianze, hakuna msanii yeyote aliyeimba English song ikawa hit bila kubabatiza. Hakuna anayenikaribia hata kwa kuongea,” Harmonize alisema kwa kukariri.
Msanii huyo ambaye kwa matamshi yake alikuwa anarejelea wimbo wake wa ‘Single Again’ alisema kuwa upeo ambao ameufikia kimuziki, hafai kuendelea kurejelewa kama msanii wa Bongo bali yeye sasa ni mwanamuziki wa kimataifa.
“Nilishakataa kuitwa msanii wa Bongo Fleva miezi kadhaa iliyopita. Naona kuna baadhi ya waandishi wa Habari wanahitaji vigezo zaidi. Hakuna yeyote ninaweza nikasimama naye kalamu kwa kalamu tukamwaga wino ukatoshana,” Harmonize alisema akirejelea uhodari wake katika uandishi wa muziki kwa Kiingereza.
Hakuishia hapo, katika mkutano mwingine na waandishi wa Habari, Harmonize alisisitiza kwamba hakukosea hata kidogo katika maandishi yake na wala hajamkosea yeyote kwa kusema vile.
‘Mimi ni staa wa kimataifa, kwani wewe unaonaje Kiingereza changu?” alimuuliza mwanahabari mmoja na kuendelea, “wewe si umehoji hoji watu wengi? Unaonaje upande wangu? Ukweli utabaki pale pale. Nimejifunza na naivchukulia hivyo na lazima niweke msimamo. Hivyo ni sharti nijivunie hilo na kama sitojivunia ina maana hata siwaheshimu nyinyi mnaonipa sapoti.”
“Kwa hiyo kama mtu akiiona kama ni negative, mimi nimezungumza tu ukweli na ndivyo ilivyo,” Harmonize aliongeza.
Kauli zake zinajiri wiki chache baada ya kudai kwamba ndiye atakuwa msanii wa kwanza kutoka Tanzania kuteuliwa kuwania tuzo ya Grammy na hata kuishinda kabisa.
Alifichua haya wakati anazungumzia sababu zake kwa nini anahisi Diamond hakufanikiwa kuingia kwenye vitabu vya Grammy, akisema kwamba ingekuwa vigumu kwake kwani wimbo wake wa Komasava hauna lolote zaidi ya salamu tu.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!