Mchungaji wa kanisa la Neno Evangelism, James Maina Ng’ang’a amezua mjadala pevu katika mitandao ya kijamii baada ya kudai kwamba lugha ya mtaani maarufu kama sheng ni ya kishetani.


Katika video moja ambayo imeibuka mitandaoni, Ng’ang’a alikuwa anazungumza na waumini wa kanisa lake alipoamua kuwapa somo kuhusu baadhi ya vitu vya kufanya na kutamka baada ya kupata wokovu.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kwa mujibu wa Ng’ang’a, mtu ukishapata wokovu, matumizi ya maneno ya lugha ya mtaani yanapaswa kuondoka kinywani kwako kabisa, kwani kuyatumia ni kama kurudi katika utumwa wa shetani.


Alitaja baadhi ya maneno hayo, akisema kuwa hajui maana yake bali huwa anayasikia aghalabu katika mazungumzo ya watu.


“Ukishaokoka tu, hicho Kiswahili cha wakora wakora kama ‘sasa uta’do manze’ hizo ni mapepo. Huwezi ongea ‘buda, manze’ sijui nini takataka. Sasa ukiongea ‘manze buda unajua mimi niko, si unipe chwani’ mimi sijui hata hiyo chwani ni nini,” Pasta Ng’ang’a aling’aka.


Mchungaji huyo aliwarai waumini katika kanisa lake kama kweli wamepokea wokovu, basi wafanye kama kawaida kuzungumza lugha ambayo inaeleweka na kila mtu.


Aliitaja lugha ya sheng’ kama lugha ya wakora.


“Sasa utazungumza lugha ambayo inaeleweka, sio lugha ya wakora.”