SIKU 5 baada ya Marioo kuachia albamu yake ya pili – The God Son, kumekuwa na maoni mseto kutoka kwa mashabiki wake lakini pia wakosoaji wa muziki.


Moja kati ya sekeseke ambazo Marioo ameamua kuzizungumzia ni uvumi unaozingira wimbo wake wa nne kwenye albamu hiyo, kolabo aliyoshirikiana na Bien kutoka Kenya.


Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Baadhi wamekuwa wakidai kwamba Marioo alimwandikia Bien mistari yake katika kolabo hiyo ya wimbo wa Nairobi.


Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari za burudani, Marioo alikanusha madai hayo akisema kwamba kila mmoja alihusika katika kujiandikia vesi yake mwenyewe.


Hata hivyo, Marioo alifafanua kwamba wakati wa uandishi wa kolabo hiyo, walikuwa wote kwenye studio.


Akitetea uamuzi wa kuwepo wote kwenye studio, Marioo alisema kwamba katika ngoma zake, yeye anatambua siri ya ngoma kuwa kali ni katika vesi ya pili ambayo inafaa kuwa kali kupita kiasi.


“Hapana sikumuandikia. Aliandika yeye mwenyewe. Lakini tulikuwepo wote studio. Unajua mimi napenda ngoma i’balance au vesi ya pili ikuwe kali zaidi. Kwa sababu ndio siri ya hit song inakuwa hapo. Vesi ya kwanza inatakiwa iwe kali lakini ya pili inatakiwa iwe kali zaidi,” Marioo alisema.


Lakini je, kwa nini vesi ya pili inatakiwa iwe kali zaidi?


Kwa mujibu wa Marioo, Vesi ya pili ikinoga, maanake itavutia watu wengi kusikiliza angalau wimbo hadi kwa asilimia 80.


“Ukali wa vesi ya pili huwavutia watu kusikiliza dakika 3 au tatu na nusu au wimbo wote. Kwa hiyo tulikuwa wote studio na aliandika yeye mwenyewe japokuwa unajua yeye ni mtu kutoka taifa tofauti kwa hivyo kuna baadhi ya vitu tulikuwa tunaulizana,” Marioo alisema.


Kwa kawaida, nyimbo nyingi huchukua kati ya dakika 3 hadi 4 mwisho.


Albamu yake ya The God Son ni ya pili katika taaluma yake ya muziki, baada ya kuachia albamu ya The Kid You Know mapema mwaka jana.


Marioo anajitambua kama msanii huru ambaye hataki kushirikishwa kwenye bifu za baadhi ya wasanii wakubwa kama vile Diamond, Alikiba na Harmonize.


Miezi michache iliyopita, Marioo alizindua rasmi msanii wake wa kwanza katika lebo yake ya Bad Nation – Stans.