MSANII Kevin Bahati Kioko alikuwa na wakati mgumu
kutoa maelezo kwa wanawe wa kike sababu ya kuvalia mavazi ya kike hali ya kuwa
yeye ni baba.
Katika klipu fupi aliyoichapisha kwenye ukurasa wake
wa Instagram, Bahati alionekana akiwa amevaa vazi la kike – linalokisiwa kuwa
la mkewe, Diana Marua.
Ghafla mabinti zake, Mueni na Heaven wakamfumania
akirekodiwa huku akijishebedua kama mwanasosholaiti kwenye vazi hilo.
Mshangao katika nyuso za mabinti wake ulishamiri,
wote wakishindwa kujizuia kufahamu ni nini kimemkuta baba yao.
Bahati alijaribu kuwaeleza mabinti hao kuwa alikuwa
anafanya hivyo, si kwa kupotoka kimaadili bali ni kwa ajili ya kutengeneza
maudhui tu, lakini nyuso za mabinti hao zilionekana kutokubali maelezo yake.
“Nani
atawaelewesha Watoto wangu kuwa Baba anatengeneza Maudhui tu???!!!”
Bahati aliandika kwenye video hiyo baada ya maelezo yake kushindwa kuwashawizi
mabinti zake.
Mabinti hao walicheka na kuanguka chini huku baba yao
akijaribu kuwashawishi kukubali kwamba ni maudhui tu anajaribu kutengeneza na
si vinginevyo.
Baada ya kicheko cha muda, mabinti zake walipata
nguvu ya kuinuka na kumkabili baba yao na maswali, “Baba kusema ukweli sasa hiki
unachofanya ni nini?”
Binti Mueni aliibua kumbukumbu kwamba hii si mara ya
kwanza kumuona babake akiwa katika mavazi ya kike kwani wakati Fulani alimuona
akiwa amevalia viatu vya visigino virefu na kumalizia kichwani na wigi la kike.
Safari hii kando na vazi la kike, Bahati alijipodoa
kwenye midomo na kubeba mkoba wa kike, katika kile mkewe alisikika akisema ni “kumalizia
muonekano wa kike mia fil mia.”
Bahati si mtu maarufu wa kwanza nchini kuonekana katika mavazi kinyume na jinsia yake.
Wengine wengi tu akiwemo Kinuthia, Eric Omondi,
Mtumba Man … wamekuwa wakizua mjadala pevu wanapovalia mavazi ya kike na hata
kujipodoa kama wanawake.
Kwa wakati mmoja, mchungaji Robert Burale aliwafokea
na kuwakemea wanaovalia mavazi kinyume na jninsi yao, haswa wanaume akiwasuta
kuwa wanapotosha jamii kimaadili.
Katika mazungumzo na Obinna mnamo Aprili mwaka huu,
Burale alisema kwamba kuvalia nguo za kike hali ya kuwa wewe ni mwanaume kwa
kauli kwamba “ni unga unatafuta” ni kujikosea heshima, lakini pia kudumisha
jinsia ya mtoto wa kiume.
"Pia anahitaji kufundishwa. Kwa nini avae kama
mwanamke, akicheza kwenye mitandao ya kijamii? Anahitaji kuambiwa ukweli.
Huwezi kwenda kufanya twerking, na wewe ni mwanaume. Anahitaji kuambiwa ukweli," Burale alisema.
Burale ni mmoja kati ya wachungaji wachache ambao katika
mahubiri yao aghalabu, hukemea vitendo vinavyoonekana kuenda kinyume na jinsia
ya mtu, akisema kwamba ni wajibu wake kufungua macho ya kizazi cha sasa ambacho
anahisi kimefumbwa na wimbo la mitandao ya kijamii.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!