MPENZI wa Marioo, Paula Kajala amefichua kwamba katika maisha yake anatamani sana Marioo amuoe rasmi katika harusi, huku akiyapa masomo nafasi ya pili katika maisha yake.

Akizungumza kwenye mahojiano na Clouds Media, Paula alisema kwamba angetaka sana kuolewa kwanza kisha masomo yaje baadae.

Alipoulizwa kuhusu elimu yake, Paula alifichua kwamba japo aliachia masomo ya fasheni njiani, ana azma ya kuenda kumalizia masomo yake pindi binti yao Amarah atakapokua.

“Nitaendelea na masomo, nasubiri Amarah akue kwanza. Hiyo inawezekana. Mimi nataka niendelee kusomea fasheni kwa sababu ndicho kitu ambacho nakipenda. Ninataka kujiendeleza kwenye hilo,” Paula Kajala alisema.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“Hata hivyo bado mipango ya ndoa naitaka sana. Nataka kuolewa kwanza masomo baadae,” aliongeza.

Marioo alipoulizwa kuhusu hoja hiyo ya mpenzi wake, alikiri kwamba ni suala la muda tu kwani sehemu kubwa wameshaifanya tayari ikiwa ni pamoja na kuonana na kujuana na wakwe, katika shughuli ya kutambulisha jinsia ya mtoto wao miezi michache kabla ya kuzaliwa kwake.

“Suala na ndoa ni jambo jema, na sisi tumeshakuwa familia. Katika vitu vilivyotokea hapa, ina maana suala la ndoa ni suala dogo sana. Ni suala tu la kuamua, na sheria tuwe tushaifuata maana vitu vingi vya msingi tumeshavifanya kwa hiyo imebakia tu sisi kusema kwamba jamani tarehe Fulani tunataka tuoane, tufunge pingu za maisha,” Marioo alikariri kauli ya mpenziwe.

“Nitamuoa kwa sababu mwanzo nampenda, pili amenizalia binti mzuri na naheshimu uamuzi wake. Kwa hivyo, kama hitaji lake ni ndoa tu hilo ni suala dogo na limeisha,” Marioo aliongeza.

Katika video ya mahojiano hayo, Paula alionekana akiwa bila kujipodoa na alipoulizwa, alisema kwamba tangu awe mzazi, hapendi kutumiwa vipodozi, akikiri kwamba hiyo ni baada ya kutambua kuwa yeye ni mrembo bila kujipodoa.

“Situmii make-up kwa sababu mimi ni mzuri tu jinsi nilivyo. Sio kama sipaki make-up, lakini natumia tu mara moja moja. Na Marioo hapendi nipake make-up. Nikipata make-up huwa ananichamba,” Paula alisema huku Marioo akitilia mkazo kwa kusema, “Mimi namuona akikaa hivyo anakuwa sawa tu. Japo naunga mkono huo urembo wa kujiongeza lakini akikaa hivi jinsi alivyo anakaa mzuri zaidi.”