UGOMVI baina ya Harmonize na Diamond kuhusu ni nani atakuwa wa kwanza kupeleka muziki wa Bongo Fleva hadi kwenye jukwaa la kimataifa ungali mbali sana na kufikia kikomo.

Hii ni baada ya Harmonize kumpiga kijembe Diamond kuhusu kutoteuliwa kuwania tuzo ya Grammy mwaka huu licha ya kuonekana kufanya ngoma zilizotambulika kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Harmonize alipoulizwa kuhusu Grammy, alisema atakuwa msanii wa kwanza Afrika Mashariki kushinda tuzo hiyo maarufu kwenye Sanaa ya muziki duniani.

Katika kile kilichoonekana kama ni kutupa kijembe kwa Diamond katika wimbo wake wa Komasava – ambayo ni njia ya kumtaka mtu salamu kwa lugha ya Kifaransa, Harmonize alidai kwamba wimbo huo haukuwa na maudhui yoyote ya kumwenzesha kushinda Grammy zaidi ya salamu tu.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Kwa mujibu wa Harmonize, Diamond asingefanikiwa hata kidogo kushinda Grammy kwa kutamka salamu kwa lugha ya Kifaransa (comment ca va) kwenye wimbo mzima wa Komasava.

“Kuzungumzia kuhusu Grammy, jibu langu litakuwa hivi: kama unazungumza kuhusu Grammy basi jua hapa mnazungumza na mshindi wa Grammy Makala ya 2025/2026. Kwa sababu mimi najua inahitaji nini ili kushinda. Huwezi shinda Grammy kwa kusalimia watu. Huwezi,” Harmonize alisema.

“Unahitaji utunzi na uzalishaji wa kipekee ili kushinda Grammy, halafu usichokijua ni kwamba wnaaoandaa Grammy hata hawajui kama wewe ni maarufu, hawajui kama unajulikana. Hivyo tujikite katika muziki, muziki wenyewe ukutangaze. Mengine hayana maana, umaarufu kwenye makamera ni vyako tu, lakini wale wanasikiliza kazi yako tu,” Harmonize aliongeza huku akisisitiza kwamba sharti awepo kwenye orodha ya wawaniaji wa tuzo hizo mwakani.

Akionyesha kutyumbishwa na uwezekano finyu wa kuteuliwa, Harmonize alisema kwamba atakuwa si tu msanii wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kuteuliwa kuwania Grammy lakini pia ataibuka mshindi na kurudi na ushindi Bongo.

Kauli yake kuhusu Grammy inajiri siku chache tu baada ya Diamond kutoa kauli yake kuhusu kutoteuliwa kuwania tuzo hizo mwaka huu licha ya ngoma yake ya Komasava aliyomshirikisha mkali kutoka Kanada, Jason Derulo kuonekana kuwavutia mashabiki wengi kutoka pembe nne za dunia.

Akijibu mashabiki wake walioonekana kusawijika nyuso kwa kukosa kuliona jina lake kwenye orodha ya wawaniaji, Diamond alisema kwamba mashabiki hawafai kukata tamaa, bali wanafaa kumpa moyo kutumia hiyo kama funzo kujiboresha zaidi katika uteuzi wa mwaka ujao.

“Tunapofeli kufanikiwa tusichukie, lazima tuongeze kasi na kuifanyia tathmini kuangalia ni sehemu gani tuliteleza,” Diamond alisema.

‘Mimi ni miongoni mwa watu tukikaa na timu yangu tusipochukua kitu chochote hatujakipata. Wakianza kulalamika sipendi. Nawaambia pale huenda kuna sehemu hatuko sawa. Pengine hatuna connection, au kuna dosari katika kazi yetu tuliyoifanya,’ aliongeza.

Diamond aliahidi kuzama kwenye studio kwa mara nyingine tena kujibidiisha katika kutoa ngoma kali alizozirejelea kama ‘mawe’ ili kuboresha nafasi yake ya kuwepo kwenye orodha ya wawaniaji wa Grammy mwaka ujao, na pengine hata kuibuka na ushindi.

“Kwa sasa hivi ni kumwaga mawe [nyimbo] mengi sana duniani. Mwenyezi Mungu atatuandikia mwakani tunaingia [Grammy] na kama hatuingii tutafika kwa pamoja ama tunaungama kwa sababu mimi naamini kwamba hakuna kisichowezekana,” alisema.