
AFISA mkuu mtendaji wa Jumuiya ya hakimiliki ya
muziki ya Kenya (MCSK), Dkt Ezekiel Mutua amevunja kimya chake, siku moja baada
ya kuenezwa kwa barua inayodai kuwa amesimamishwa kazi.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Mutua alichapisha
taarifa ndefu akipuuzilia mbali taarifa hizo kama uvumi feki unaonuia kuchafua
jina lake.
Dkt Mutua alisema kwamba watu wanaodai kuwa wanachama
wa kamati kuu ya MCSK wote hawajui na kufichua kuwa tayari yuko ofisini
kushughulikia uvumi huo alioutaja kama propaganda mbaya.
Mutua alisema kwamba wikendi iliyopita alikuwa nchini
DRC na baadae kurejea nchini kwa shughuli nyingine na hivyo alishangazwa sana
kuona uvumi mitandaoni kwamba amesimamishwa kazi.
“Kwa hiyo ilishangaza kwangu kujua baadaye kwamba nilipokuwa
nikishughulika sana kutekeleza jukumu langu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya
ya Hakimiliki ya Muziki ya Kenya mtu fulani alikuwa akieneza propaganda mbaya
kuhusu madai ya kuachishwa kazi kwangu, au ilikuwa ni kusimamishwa kazi?”
Mutua alihoji.
CEO huyo alithibitisha kwamba bado yuko ofisini kama afisa
mkuu mtendaji wa MCSK, akiwataka wanablogu wanaoeneza uvumi wa kusimamishwa
kwake kazi kufanya haki kwa kutembea ofisini kupata ukweli kamili kutoka kwake.
Hata hivyo, Mutua alithibitisha kwamba kuna vuta-nikuvute
katika uongozi wa MCSK lakini akasema kuwa mzozo huo haufikii cheo chake bali
unaishia katika vyeo vya wanachama waliochaguliwa tu.
“Ni kweli kwamba kuna mizozo ya uongozi katika MCSK lakini inagusa tu
Wakurugenzi walio na nyadhifa zisizo za watendaji waliochaguliwa. Mkurugenzi
Mtendaji na wafanyakazi hawajachaguliwa na kuna taratibu za wazi za hatua za
kinidhamu,” alisema.
Mutua alifichua kwamba leo alifaa kuwa na mkutano nje ya
ofisini lakini ikambidi kusalia ofisini ili kumaliza kabisa ukungu unaozingira
uvumi wa kusimamishwa kwake kazi, akisema kuwa tayari amewaarifu mawakili wake
kuchukua hatua madhubuti za kisheria.
“Nilipaswa kuwa kwenye mikutano nje ya ofisi leo lakini ilinibidi
kughairi na kubaki ili kushughulikia propaganda fulani. Kama msemo
unavyokwenda, "kitu pekee cha lazima kwa ushindi wa uovu ni kwa watu wema
kufanya chochote." Nimewaelekeza wanasheria wangu ipasavyo,” Mutua
alikiri.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!