TIMU ya taifa ya Kenya kwa vijana wasiozidi umri wa miaka 20 wanatarajiwa kuchuana na timu ya Tottenham ya UIngereza ya vijana wasiozidi umri wa miaka 23 katika mechi mbili za kirafiki.

Haya ni kwa mujibu wa naibu Kamishna Mkuu wa Kenya katika jimbo la St. James mjini London, Joseph Warui.

Warui alitangaza mipango ya kuandaa mechi ya kirafiki kati ya timu ya taifa ya Kenya U20 na Tottenham Hotspur U23 ambayo itachezwa kwa mikondo miwili, moja nchini Uingereza na nyingine Uturuki.

Warui alitangaza hayo baada ya kukutana na nahodha wa zamani wa Harambee Stars Victor Wanyama jijini London siku ya Jumatatu.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Wawili hao walijadili mada mbalimbali, ikiwemo uwezekano wa Kenya kucheza na Tottenham nchini Uingereza na Asia.

Hata hivyo, hakuthibitisha iwapo Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) lilihusika katika majadiliano hayo.

Wanyama ambaye ni kiungo wa zamani wa Tottenham Hotspur, aliyekaa miaka minne katika klabu hiyo ya Kaskazini mwa London alikuwa muhimu katika kuongoza mijadala ya kuandaa mechi ya maonyesho.

"Tunaandaa mechi ya kirafiki mnamo Desemba kati ya Timu ya Taifa ya U20 ya Kenya na Tottenham Hotspur U23 nchini Uturuki na Uingereza," Warui alisema katika taarifa.

Mechi hii ya kirafiki itakuwa ya manufaa kwa timu ya Kenya ya U20 inapojiandaa kwa Kombe la Mataifa ya Afrika U20 (AFCON) mwaka ujao, ambayo pia itatumika kama kufuzu kwa Kombe la Dunia la U20 nchini Chile.

Huku timu ya wakubwa Harambee Stars ikiwa inasuasua hadi kubanduliwa nje ya mashindano ya AFCON mwakani nchini Morocco, vijana wa Rising Stars na kina dada wasiozidi umri wa miaka 17 wa Harambee Starlets wamesalia kuwa wa pekee kuipeperusha bendera ya Kenya katika mashindano ya kimataifa.

Itakumbukwa Rising Stars walitinga kwenye fainali ya CECAFA ambapo walichapwa mabao 2-1 na Tanzania.

Kwa upande mwingine, wasichana wasiozidi umri wa miaka 17 walikuwa timu ya taifa ya kwanza kutoka Kenya kufuzu katika mashindano ya kombe la dunia.

Mashindano hayo yalifanyika katika jamhuri ya Dominika ambapo wasichana hao walishinda mechi moja tu kwenye kundi lao dhidi ya Mexico.