KWA mara ya kwanza, msanii Diamond Platnumz amefunguka kuhusu kukosa kuteuliwa kuwania tuzo katika kitengo chochote cha tuzo kubwa za Sanaa duniani za Grammy.

Akizungumza na waandishi wa habari za burudani katika kikao cha kuzindua kampeni ya chapa moja ya pombe nchini Tanzania, Diamond alisema kwamba hapendi kuona mashabiki wake wakitoa kauli za kukata tamaa pindi wanaposhindwa kukipata walichokuwa wakikitarajia.

Alisema kwamba siku zote katika maisha yake kwenye muziki, yeye ni mtu anayeaminia sana katika kufanya kazi bila kujali ni nini watu watasema huko nje.

Msanii huyo alifichua kwamba yeye baada ya kukosa kuteuliwa kuwania Grammy, ilikuja kwake kama motisha ya kuachia ngoma kali hata zaidi akilenga tuzo za mwaka ujao.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

“La kwanza mimi kama msanii jukumu mkubwa ni vkuhakikisha nafanya kazi iliyo bora kuniingiza kwenye mashindano. Na kwenye mashindano pale ni lazima tukubali kwamba si kila wakati wowote unaweza ukafanikiwa.”

“Na tunapofeli kufanikiwa tusichukie, lazima tuongeze kasi na kuifanyia tathmini kuangalia ni sehemu gani tuliteleza,” Diamond alisema.

‘Mimi ni miongoni mwa watu tukikaa na timu yangu tusipochukua kitu chochote hatujakipata. Wakianza kulalamika sipendi. Nawaambia pale huenda kuna sehemu hatuko sawa. Pengine hatuna connection, au kuna dosari katika kazi yetu tuliyoifanya,’ aliongeza..

Msanii huyo alimalizia akisema kwamba katika kila kitu mtu yeyote anayefanya, matokeo yake lazima amuamini Mungu kwamba yeye kapanga matokeo yawe jinsi yalivyotukia.

“Kwa hiyo lazima ukubali kitu kinapotokea Mwenyezi Mungu ndiye kakipanga. Na kisikukatishe tamaa ukaanza kutukana watu kwa sababu haya mambo yashapitwa na wakati. Jitathmini mwenyewe, toa goma lingine na baadae mambo yatanyooka,” alishauri.

Diamond alisema kwamba si yeye tu am baye alikosa tuzo licha ya kufanya kazi nzuri, akisema wapo wasanii wengi tu kama yeye ambao walikosa kuingia kwenye orodha ya Grammy.

“Kuna watu wengi tu ambao hawakupata na walikuwa na kazi bora. Kwa hiyo sisi tuamini tumefanya kazi iliyokuwa bora na tumepata mawazo mazuri ya kufungua dunia. Kwa sasa hivi ni kumwaga mawe [nyimbo] mengi sana duniani. Mwenyezi Mungu atatuandikia mwakani tunaingia [Grammy] na kama hatuingii tutafika kwa pamoja ama tunaungama kwa sababu mimi naamini kwamba hakuna kisichowezekana,” alimaliza.