
Kocha mkuu wa Gor Mahia FC aliyetimuliwa Leonardo Neiva amehusisha matatizo yake katika klabu hiyo na mizozo ya kisiasa.
Raia huyo wa Brazil alidai aliihama klabu hiyo kwa sababu za kiusalama baada ya mashabiki waliokasirika kumkabili mara mbili kufuatia msururu wa matokeo yasiyoridhisha katika Ligi Kuu ya Kenya.
Gor Mahia ilithibitisha kuondoka kwa kocha huyo mnamo Jumatano, Novemba 13, ikinukuu kipengele cha mkataba kilichowaruhusu kuachana.
Uamuzi huo ulikuja baada ya mechi sita pekee za ligi, na kuiacha klabu hiyo ikiwa katika nafasi ya 12 kwenye jedwali la timu 18.
"Niliondoka kwenye klabu kwa sababu ya usalama wangu na uadilifu wangu," Neiva alifichua katika taarifa.
"Ni 2024, na kwa bahati mbaya, hii bado inatokea kwenye mpira wa miguu. Masuala ya kisiasa, mwaka wa uchaguzi na maswali mengine yanaingilia moja kwa moja maisha yetu ya kila siku.”
Mashabiki waliojawa na hasira walimkabili Neiva kueleza kutoridhishwa kwao na uchezaji wa timu hiyo, wakitaka ajiuzulu na kumlazimisha kuondoka Uwanja wa Machakos chini ya ulinzi mkali.
Matatizo yalianza pale Gor ilipofungwa 2-1 na Nairobi City Stars katika uwanja wa Kenyatta mjini Machakos. Matokeo yaliyofuata, ikiwa ni pamoja na sare ya 2-2 na Murang’a Seal na kufungwa 2-0 na Bandari, yalichochea ghasia miongoni mwa wafuasi.
"Kufukuzwa kwangu kumechochewa kisiasa, kila mtu anafahamu kuwa vitendo vyao vilipangwa. Watu 10 hadi 15 walinivamia kwa nyakati mbili tofauti, na ningependa kufafanua kuwa ni tukio lililopangwa. Walikuwa wanafahamu lengo lao na wanachotamani," Neiva alisema.
Licha ya machafuko hayo, Neiva alisisitiza kuwa bado ana uhusiano mzuri na uongozi wa klabu hiyo.
“Ninashukuru sana jinsi mwenyekiti wa klabu Ambrose alivyonitendea tangu siku yangu ya kwanza kazini hadi tulipoachana. Nilifurahia kufanya kazi na Gor Mahia," alibainisha.
Katika kipindi kifupi cha uongozi wake, Gor Mahia ilirekodi matokeo ya wastani. Walishinda mechi mbili za ligi, sare mara mbili, na pia kupoteza mara mbili. Pia walishindwa na Al Ahly ya Misri katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Hata hivyo, alikiri kuondoka kwake kunaweza kuchochewa na wasiwasi wa utendakazi.
"Hakuna kitu maalum. Labda ilihusiana na matokeo, lakini hii ni mpira wa miguu. Sina mamlaka juu ya uamuzi wao."
Neiva alikanusha madai kwenye mitandao ya kijamii kwamba mmoja wa wasaidizi wake alihusika katika kuandaa mashambulizi dhidi yake. Ingawa muda wake uliisha ghafla, Neiva bado ana matumaini kuhusu uwezekano wa Gor Mahia msimu huu.
"Hakika wanaweza kushinda taji kwa mara nyingine tena. Pamoja na vifaa bora zaidi, wana wachezaji bora katika taifa. Wana wafanyikazi wa kiufundi wenye nguvu wanaojua kushinda," alisema.
Neiva pia alifichua kuwa alikataa ofa kutoka Asia na Indonesia alipokuwa Gor Mahia. "Nilitarajia kushinda mataji mengi zaidi, kujaribu kushikilia taji, na kukaa nao kwa muda mrefu," alisema.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!