Wachezaji wa AFC Leopards
Imeibuka kuwa vigogo wa soka nchini, AFC Leopards, wanakabiliwa na wakati mgumu wa kuwalipa wachezaji wao kutokana na matatizo makubwa ya kifedha.

Uongozi wa klabu hiyo ulisema utamudu tu kulipa sehemu ya mishahara ya Oktoba ya wachezaji wake na benchi la ufundi, huku wakiahidi kulipa deni lililosalia baadaye.

"Ofisi imeweza kupata pesa kugharamia sehemu ya mishahara yetu ya Oktoba. Tafadhali fahamu kuwa huu sio mshahara wote, lakini utatusaidia kupata hadi malimbikizo yalipwe," wasimamizi walisema kupitia taarifa iliyotolewa Ijumaa.

Msururu wa matokeo duni na kushindwa kulipa madeni yaliyosalia, kumeweka uongozi wa Dan Shikanda chini ya shinikizo kubwa.

Mashabiki kwenye mitandao ya kijamii wamepaza sauti wakiitaka klabu hiyo kushughulikia tatizo hilo la fedha.

Mlezi wa AFC Leopards Alex Muteshi alikiri hali mbaya ya kifedha ya klabu hiyo na kusema walikuwa wakitafuta njia mbadala za kujikimu.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Muteshi pia alifichua kuwa klabu haikuweza kuilipa Mafro Sports salio lililobaki la dola za Kimarekani 32,000 kwa ajili ya vifaa.

"Tunatatizika kifedha. Itakuwa vigumu kwetu kuheshimu kandarasi kutokana na uhaba wa fedha," Muteshi alisema.

"Tunadaiwa dola za Kimarekani 32,000, pamoja na ada ya ziada ya ghala ya zaidi ya dola 5,000. Hata hivyo, tuko tayari kujadiliana nao kuhusu namna bora ya kusuluhisha suala hili.”

Muteshi alipendekeza kuwa Mafro inaweza kuuza jezi na vifaa vya kuiga ili kurejesha pesa zao ndani ya miezi miwili, akieleza kuwa klabu hiyo tayari ilikuwa imemjulisha mtengenezaji kuhusu matatizo yao ya kifedha.

"Nimewashauri Mafro kuleta jezi na kuziuza. Tunafanya kila tuwezalo kutatua hali hiyo."

Uwanjani, AFC Leopards wametatizika umudu hadhi yao kama vigogo wa soka nchini.

Baada ya kuanza msimu kwa hali chanya, timu hiyo haijapata ushindi katika mechi nne zilizopita.

Leopards wametoka sare dhidi ya Mara Sugar na Kariobangi Sharks, na kushindwa na Murang'a Seal na Ulinzi Stars.

Msururu wa matokeo yasiyoridhisha umewafanya mashabiki kumshinikiza kocha mkuu Tomas Trucha kujiuzulu.

Klabu hiyo kwa sasa inajiandaa kumenyana na wapinzani wao Gor Mahia katika pambano kali la Mashemeji Derby litakalofanyika baada ya mapumziko ya kimataifa ya Novemba.