
Klabu ya Ligi Kuu ya Kenya Mara Sugar, wamemtimua mkurugenzi wao wa kiufundi Bonface Ambani.
Siku ya Ijumaa, klabu hiyo ilitangaza uamuzi wa kukata uhusiano na Ambani kwenye ukurasa wake wa Facebook.
"Tunatangaza kumalizika kwa mazungumzo na mkurugenzi wetu wa ufundi Bonface Ambani. Tunamshukuru kwa huduma yake na tunamtakia mafanikio anapoondoka Mara Sugar FC akiangazia changamoto nyingine," ilisema taarifa ya klabu hiyo.
Hakukuwa na dalili za nyufa klabuni hapo kutokana na mwanzo mzuri wa timu hiyo msimu huu.
Vilevile Ambani aliwalimbikizia sifa tele uongozi, benchi la ufundi na kitengo cha uchezaji cha Mara Sugar.
Hivi majuzi, Ambani alifichua kuwa klabu hiyo ilikuwa na mpango wa kujenga uwanja mdogo wa Enoosaen ili kupunguza mzigo wa kifedha wa kusafiri kwa mechi za nyumbani na ugenini.
Pia alidai kuwa timu hiyo ilikuwa na lengo la kutwaa ubingwa wa ligi hiyo licha ya kuwa na wachezaji wengi wasio na uzeofu unaohitajika.
Hapo awali Ambani aliwahi kuwa kocha mkuu wa AFC Leopards Youth na kugundua wachezaji wenye vipaji, akiwemo kiungo wa Harambee Stars na Gor Mahia Austin Odhiambo.
Ambani aliichezea Tusker FC kwa misimu miwili na kushinda tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Kenya mwaka wa 2006 baada ya kupachika mabao 20.
Baadaye alijiunga na klabu ya India East Bengal mwanzoni mwa 2006 na akatumia msimu wake wa mwisho katika klabu ya Tanzania Young Africans, ambapo alifunga mabao 18 katika mechi 22.
Jeraha la mishipa ya Achilles lilimlazimisha kustaafu mapema mnamo 2010.
Comments 0
Sign in to join the conversation
Sign In Create AccountNo comments yet. Be the first to share your thoughts!