Makamu wa rais wa zamani wa Kenya Kalonzo Musyoka mnamo Alhamisi alikutana na familia ya marehemu mtayarishaji maudhui Tabitha Gatwiri ambaye kwa bahati mbaya alipoteza maisha wiki jana.

Kalonzo aliandamana na aliyekuwa gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, seneta wa Kitui Enoch Wambua, viongozi wengine wa Kaunti ya Nairobi na wasanii kadhaa walipokutana na familia ya marehemu Gatwiri jijini Nairobi.

Katika taarifa, kiongozi huyo wa Chama cha Wiper alibainisha kuwa madhumuni ya mkutano wake na familia ya Gatwiri ilikuwa kuwasilisha rambirambi zake. Pia alitumia fursa hiyo kutambua kipawa cha marehemu mtayarishaji huyo wa maudhui na kuzungumzia jinsi kilivyoathiri Wakenya wengine.

“Gatwiri alikuwa na kipawa kikubwa, kama nilivyomwambia kakake Brian na baba Robert Kirimi. Kuomboleza kwa huzuni na uchungu kote ulimwenguni kunaonyesha jinsi talanta za Gatwiri zilivyoathiri idadi kubwa ya watu,” Kalonzo alisema Alhamisi jioni.

Aliongeza, "Sekta ya ubunifu imepoteza mtayarishaji wa maudhui muhimu, na ninamshukuru Alex Mathenge almaarufu "Security Engineer", MCA Tricky, Naomi Kuria, na Shipira kwa kusimama na familia katika wakati huu mgumu zaidi.

Enjoying this article? Subscribe for unlimited access to premium sports coverage.
View Plans

Mwanasiasa huyo mkongwe pia aliwataka Wakenya kuendelea kukumbuka jinsi marehemu Gatwiri alivyowatumbuiza kwa talanta yake.

Huku haya yakiendelea,  imebainika kwamba Gatwiri atazikwa siku ya Ijumaa, Novemba 15, 2024, familia yake ilifichua.

Bango lililochapishwa na mchekeshaji Alex Mathenge linaonyesha kuwa mwanadada huyo aliyeaga dunia wiki jana akiwa na umri wa miaka 29 atazikwa katika kaunti ya Meru.

Mikutano ya kupanga mazishi ya marehemu Gatwiri inaendelea kila siku katika Ukumbi wa hoteli ya The Blue Spring kuanzia saa kumi alasiri na saa moja jioni.